Header Ads Widget

WAZIRI WA FEDHA DKT MWIGULU NCHEMBA NA WAZIRI WA MAJI JUMAA AWESO WASHUHUDIA UTIAJI SAINI MRADI WA MAJI USHETU

 Wakionyesha nyaraka zilizotiwa saini tayari kwa kuanza mradi wa maji.

Na Frank Mshana,Ushetu 

WAZIRI wa fedha Dkt  Mwigulu Nchemba  na Waziri wa maji   Mhe. Jumaa  leo wameshuhudia hafla ya utiaji saini mradi mkubwa wa maji wa zaidi ya Bilioni 44 katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Mradi huo utaanza utekelezaji hivi karibuni na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 24.

 

Utekelezaji wa mradi huo utahusisha Ujenzi wa matanki matatu (3) yenye ujazo wa lita 500,000; 300,000 na 100,000 katika maeneo tofauti ndani ya Kata ya Ulowa.

Pili itahusisha Ujenzi wa bomba kuu aina ya chuma lenye kipenyo cha kuanzia milimita 350 hadi milimita 100 lenye urefu wa kilometa 76 kutoka Manispaa ya Kahama kwenda Ulowa hadi kwenye matanki.

 

Pia itahusisha ujenzi wa mfumo wa kutibu maji na ujenzi wa vituo 35 vya kuchotea maji.

Ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji wenye bomba aina HDPE zenye urefu wa KM 74 pamoja na vituo vya kuchotea maji 35.

Pamoja na uunganishaji wa wateja wa majumbani 1,000 wa awali kwa wateja wa majumbani.

Ili kufanya mradi kuwa endelevu, mradi pia utahusisha ujenzi wa jengo la ofisi kwa ajili ya Chombo kitakachoundwa kuendesha mradi na kuwahudumia wananchi baada ya mradi kukamilika na kutakuwepo na ununuzi wa magari mawili (2) na pikipiki mbili (2).

 Pamoja na ununuzi wa seti moja (1) ya vitendeakazi vya msingi vya mafundi bomba pamoja na mashine moja (1) ya kuunganisha bomba aina ya HDPE. Vitendeakazi hivyo na mshine vitatumika kwenye shughuli mbalimbali za matengenezo ya mradi wakati wa uendeshaji.

 

Mradi huu utatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya SIHOTECH ENGINEERING COMPANY LTD ya Jijini Dar Es Salaam kwa kushirikiana na Kampuni ya MPONELA CONSTRUCTION COMPANY LTD ya Iringa. Gharama za Mkataba ni jumla ya *Shilingi 44,271,886,678.17.*

Manufaa ya mradi huu ni pamoja na kuboresha afya ya wananchi,  utachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Halmashauri ya Ushetu kwani utatoa fursa kwa wananchi kujihusisha na shughuli zingine za kiuchumi badala ya kutumia muda mrefu kutafuta maji, kama inavyofanyika sasa. Mradi huu pia utakuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi. 

Mradi huu umesanifiwa kuhudumia watu wapatao 189,836 wa Kata za Igunda, Kisuke, Kinamapula, Nyamilangano, Mapamba, Uyogo, Bukomela, Ushetu na Ulowa.

 Kupatikana kwa huduma ya maji safi, salama na ya uhakika katika Kata hizo kutaongeza upatikanaji wa maji kufikia kiwango kinachoendana na lengo la Serikali la asilimia 85.



 

Post a Comment

0 Comments