CHIFU KABILA LA WAKAMBA KUTOKA KENYA DK AUGUSTUS MULI APONGEZA TAMASHA LA UTAMADUNI KABILA LA WASUKUMA SANJO YA BUSIYA WILAYANI KISHAPU

Chifu Kabila la Wakamba kutoka Kenya Dk.Augustus Muli apongeza Tamasha la Utamaduni la Kabila la Wasukuma Sanjo ya Busiya wilayani Kishapu

Na Marco Maduhu,KISHAPU
CHIFU kutoka nchini Kenya
Kaunti ya Kitui wa Kabila la Wakamba Dk.Augustus Muli, amepongeza Tamasha la Utamaduni wa kabila la wasukuma Sanjo ya Busiya, kwa kuenzi mila na desturi pamoja na kuwarithisha vijana tamaduni hizo.

Ametoa pongezi hizo leo Julai 7,2024 alipokuwa Mgeni Rasmi wakati wa kuhitimisha tamasha hilo,ambalo hufanyika kila mwaka mwezi Julai hadi siku ya Saba Saba katika Ikulu ya Chifu Makwaia Negezi wilayani Kishapu.
Amesema Matamasha kama hayo ni muhimu, sababu yanawafanya watu kuwa wamoja na kuenzi tamaduni zao na kwamba wamefurahi kualikwa kwenye tamasha hilo la Kabila la wasukuma ambapo wamejifunza mambo mengi pamoja na kuona vijana wakirithishwa tamaduni zao.

"Tunafurahi kualikwa kwenye tamasha hili la Sanjo ya Busiya na Chifu Edward Makwaia na kuona utamaduni wa Kisukuma, sisi Wakamba na Wasukuma ni ndugu sasa tulioana na majina yetu yanaingiliana,na tukakuja kuwaalika pia mje Kenya,"amesema Chifu
 Muli.
"Tunaipongeza pia Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono masuala ya utamaduni,na hapa leo naona viongozi wakubwa wa Serikali akiwamo na Mkuu wa Mkoa, na sisi tutakwenda kufikisha ujumbe kwa Serikali yetu," ameongeza Chifu Muli.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amepongeza tamasha hilo la utamaduni,kwamba linadumisha mila na desturi, na hivyo kuwaomba Machifu kwamba wawarithishe vijana mila zenye kulinda maadili.
"Serikali haina ukabila,lakini ina makabila mbalimbali ambapo wananchi huenzi mila na desturi zao," amesema Macha.

"Nawaomba Machifu mila potofu muziweke kando lakini zile mila nzuri tuzienzi na kuwarithisha vijana ili kuzuia Mmomonyo wa maadili ya vijana," ameongeza Macha.

Aidha,Mkuu wa Mkoa ametoa pia Salamu za Chifu Hangaya Rais Samia kwenye Tamasha hilo,huku akiwasihi wananchi wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao utafanyika mwaka huu.
"Machifu washawishini vijana na akina mama wenyesifa, wajitokeze kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na uchaguzi Mkuu mwakani, lakini nafasi ya Rais tumuachie Rais wetu Samia Suluhu Hassan sababu anatosha na ametuletea maendeleo makubwa," amesema Macha.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo naye amepongeza tmasha hilo la utamaduni, kwamba limekuwa na faida sana kwa kuwakutanisha Wasukuma na kuenzi tamaduni zao.
Naye Chifu Edward Makwaia wa Sanjo ya Busiya, amesema kila mwaka hua wanaandaa tamasha hilo la kitamaduni kuanzia mwezi Julai na kuhitimishwa siku ya Saba Saba, ambapo pia Serikali hutumia fursa ya kusukuma ajenda zake mbalimbali kwa kufikisha ujumbe kwa wananchi.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI👇👇
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464