MTOTO WA MIEZI 9 ALIYEIBWA KAHAMA APATIKANA APELEKWA HOSPITALI KUCHUNGUZWA AFYA YAKE


MTOTO WA MIEZI 9 ALIYEIBWA KAHAMA APATIKANA APELEKWA HOSPITALI KUCHUNGUZWA AFYA YAKE

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MTOTO mwenye umri miezi 9 Meresiana Paschal,ambaye aliibwa katika Stendi ya Mabasi Manzese wilaya Kahama mkoani Shinyanga,amepatikana mkoani Geita akidaiwa kuwa na Binti Maduki Sabuni mwenye umri wa miaka (16),ambapo mtoto huyo amepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake, kabla ya kukabidhiwa kwa mama yake mzazi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo Julai 22,2024 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema Julai 18 mwaka huu,maeneo ya manzese wilayani Kahama mkoani Shinyanga,kulitokea tukio la mtoto kuibiwa aliyefahamika kwa jina la Meresiana Paschal mwenye umri wa miaezi 9 wakati mama yake Magdalena Sulas (23) akiendelea na shughuli za utafutaji riziki katika stendi hiyo ya mabasi yaendayo kakola, ambapo mtu aliyemuiba mtoto huyo alikimbia kusikojulikana.

Amesema Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za wizi wa mtoto huyo, lilianza kufanya upelelezi na kwamba Julai 21 mwaka huu, huko maeneo ya ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita, walifanikiwa kumkamata binti Maduki Sabuni (16) akiwa na mtoto huyo.

“Polisi tulifanya mahojiano ya awali na binti huyu Maduki Nyembe Sabuni, na amekiri kutenda kosa la kuiba mtoto huyo na bado tunaendelea kumhoji zaidi,”amesema Magomi.

Amesema mtoto huyo amepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya zaidi kabla ya kumkabidhi kwa mama yake mzazi.

Ametoa wito pia kwa wazazi mkoani Shinyanga, kwamba wawe na uangalizi wa karibu kwa watoto wao.

Aidha,Kamanda amekema vikali na kutoa onyo kwa mtu au watu ambao wamekuwa wakihusika na vitendo vya wizi wa watoto, sababu katika Mkoa wa Shinyanga tukio la namna hiyo ni la pili kutokea, na kwamba hatua kali za kesheria zitachukuliwa dhidi ya watu watakaondelea kuhusika na matukio hayo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464