MADIWANI SHINYANGA WALAUMU WAKANDARASI UCHELEWESHAJI MIRADI UJENZI WA BARABARA

Madiwani Shinyanga Walaumu Wakandarasi kwa Ucheleweshaji wa Miradi ya TARURA

Na Mwandishi wetu,SHINYANGA
MADIWANI wa Manispaa ya Shinyanga wameibua malalamiko makali dhidi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara za TARURA, wakidai kuwa miradi mingi inakabiliwa na ucheleweshaji mkubwa.
Katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika leo, Julai 30, waheshimiwa madiwani walitoa wito kwa wakandarasi kumaliza miradi yao kwa wakati. Mhe. Peter Koliba, Diwani wa kata ya Masekelo, alieleza wasiwasi wake kuhusu kivuko muhimu kinachounganisha kata za Mwamala Masekelo, Ibinzamata, Kitangili, na Kizumbi. Alisema kwamba kivuko hicho kilikuwa na matukio ya maafa mwaka 2015, na licha ya barua ya kuanza matengenezo iliyotolewa tarehe 26/06/2024, hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

Diwani wa kata ya Kizumbi, Mhe. Ruben Kitinya, alihoji kuhusu mradi uliopewa kampuni ya UK, akisema kwamba mkataba umekwisha tangu tarehe 29/07/2024 lakini kazi haijaisha. Aliuliza hatua zitakazochukuliwa ili wananchi wapate huduma ya barabara kwa haraka.
Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Yohana William, alifafanua kuwa mwaka wa fedha 2023/2024 walitengewa shilingi bilioni 2.9, lakini fedha zilizopatikana na kutumika ni milioni mia moja pekee, hali inayochangia ucheleweshaji wa miradi.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Elias Masumbuko, alisema tatizo la ucheleweshaji linatokana na wakandarasi kutolipwa stahiki zao. Alipongeza TARURA kwa kazi yake katika mazingira haya magumu na kuomba ushirikiano wa haraka ili kuondoa kero hizi kwa wananchi.
Baraza la madiwani manispaa ya Shinyanga likiendelea.





          Baraza la madiwani                           likiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464