SHINYANGA RS YAFANYA KIKAO CHA MAELEKEZO YA UTEKELEZAJI NA USIMAMIZI WA MRADI WA GPE - TSP 2024/2025 KWA NGAZI YA MKOA NA HALMASHAURI ZAKE


SHINYANGA RS YAFANYA KIKAO CHA MAELEKEZO YA UTEKELEZAJI NA USIMAMIZI WA MRADI WA GPE - TSP 2024/2025 KWA NGAZI YA MKOA NA HALMASHAURI ZAKE

Na. Paul Kasembo, SHY RS.
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kupitia kwa Mratibu wa Mradi wa Program ya Uboreshaji Kada ya Ualimu GPE - TSP Bi. Fausta Luoga imefanya kikao na MaafisaElimu Divisheni ya Awali na Msingi , Waratibu wa mradi , Maafisa Ununuzi na Wahandisi katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri zake zote sita (6) yenye lengo la kutoa Maelekezo ya utekelezaji na usimamizi wa mradi huu unaotarajiwa kuanza rasmi Agosti, 2024.

Akizungumza wakati wa kikao hiki Bi Fausta amesema GPE TSP ni mpango unaolenga kuboresha ubora wa elimu nchini Tanzania na kwamba Mpango huo  unafadhiliwa na Ushirika wa kimataifa wa kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani. (The Global Partnership for Education) na Malengo ya programu hiyo ni kuboresha ubora wa elimu,pili kuimarisha kada ya Ualimu tatu,kuongeza usawa wa kijinsi na nne, kuimarisha ujumuishi.
Alieleza kuwa Usimamizi wa mradi huu umegawanyika katika maeneo matatu.Eneo la kwanza usimamizi wa Programu , pili uwasilishaji wa taarifa na tatu ukusanyaji wa taarifa. Huku akiwasisitiza waratibu kwenda kufanya vikao katika ngazi ya shule na jamii ili wawe na uelewa wa kutosha kuhusu utekelezaji na usimamizi wa mradi.

Pia alisisitiza kutumia Maafisa habari na vyombo vya habari kwa lengo la kutoa habari kwa wananchi ambao kimsingi ndiyo wanufaika wa miradi hii.
"Wataalam wenzangu, twendeni tukafanye vikao na mikutano tukishirikiana na Maafisa habari na vyombo vya habari ili kuweza kutoa habari kwa wananchi kwa haraka, na pia kutumia mitandao ya kijamii kuielezea miradi yetu ili watu wengi wafahamu jitihada zinazofanyika na Serikali yetu ya awamu ya sita kupitia Mh.Rais wetu dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali yetu tukufu ili lengo la Serikali liweze kufikiwa," amesema Bi. Fausta.

Kwa upande wake muwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Elimu na Ufundi ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Shinyanga Ndg. Richard Mfugale amesema kuwa shughuli zitakazotekelezwa na GPE - TSP ni pamoja na ununuzi wa vifaa visaidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, uanzishwaji wa madarasa janja kwa ajili ya ufundishaji mubashara.
Shughuli nyingine ni uchambuzi wa hali halisi ya mifumo inayokusanya taarifa za walimu, uhusishanaji wa mifumo inayokusanya taarifa za walimu, ujenzi wa nyumba za walimu 100 na ujenzi wa vituo vya walimu 150.

Kwa Mkoa wa Shinyanga Mradi utatekeleza ujenzi wa nyumba za walimu 18 na Vituo vya Walimu (TRC) 7.
Utekelezaji wa program hii ni wa muda wa miaka minne kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2026/2027.





















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464