Header Ads Widget

SHIRIKA LA THPS LAWAUNGANISHA WATU 4,077 WENYE VVU NA HUDUMA YA TIBA NA MATUNZO


Shirika la THPS lawaunganisha watu elfu 4,077 wenye VVU na huduma ya tiba na matunzo

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Meneja programu wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dk.Amos Scott.

SHIRIKA la THPS kupitia mradi wa afya hatua kwa kushirikiana na Serikali,wameweza kupima watu 211,763 virusi vya ukimwi, na kubainika watu 4,077 kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi,na kisha kuwaunganisha na huduma za tiba na matunzo.

Takwimu hizo ni zakuanzia Oktoba 2023 hadi juni 2024, ambapo THPS wanatekeleza mradi wa afya hatua, kwa ufadhili wa mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia kituo cha kidhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani (CDC).
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza katika banda la THPS.

Hayo yamebainisha leo Julai 25,2024 na Meneja programu wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dk.Amos Scott, amesema hayo kwenye zoezi la upimaji wananchi magonjwa bure (afya code clinic) lililoratibiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Kampuni ya Jambo group Limited, linalofanyika katika viwanja vya CCM Kambarage Manispaa ya Shinyanga, ambalo litakwenda hadi Julai 27 mwaka huu..

Amesema mradi huo wa afya hatua THPS wanautekeleza katika mikoa minne ambayo ni Tanga,Kigoma,pwani pamoja na Shinyanga, na wanatoa huduma za Saratani ya mlango wa kizazi,matiti,tohara, na upimaji wa virusi vya ukimwi.
"Elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi tunatoa mwaka wa tatu sasa na tuna vituo 92 vya tiba na matunzo kwa Mkoa wa Shinyanga chini ya mradi wa afya hatua,na watu ambao wanabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi wanapewa dawa za kufubaza makali na mpaka sasa watu 71,183 wanatumia dawa za ARV,"amesema Dk.Scott.

Aidha,amesema kwa upande wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi, kwamba Oktoba 2023 hadi Juni 2024 waliwafanyia uchunguzi wanawake 21,759,na 563 waligundulika kuwa na viashiria vya saratani hiyo huku 552 kati yao walipatiwa matibabu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, akiwa katika banda la THPS, amewapongeza wadau hao kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuimarisha afya za wananchi pamoja na kuwapatia elimu ya kujikinga na maradhi mbalimbali.

Ametoa wito kwa wananchi kwamba waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ukimwi sababu bado upo, pamoja na kupata tohara,na wale ambao wanagundulika kuwa na virusi vya ukimwi,wafuate masharti ikiwamo na matumizi sahihi ya dawa ya kufubaza makali ili waishi miaka mingi.

Pia,amewasisitiza waendelee kupima afya zao mara kwa mara,pamoja na kufuata ushauri wa watalaamu wa afya na kulinda afya zao.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akiwa katika Banda la THPS.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akiwa katika Banda la THPS.
Huduma zikiendelea katika Banda la THPS.

Post a Comment

0 Comments