ZAMDA SHABANI ASHINDA KWA KISHINDO UNAIBU MEYA MANISPAA YA SHINYANGA KWA ASILIMIA 100
DIWANI wa kata ya Ndala Zamda Shabani ameibuka tena mshindi katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa asilimia 100, baada ya kupata kura zote 19 zilizopigwa.
Uchaguzi huo ulifanyika leo Julai 31 katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna, na Diwani huyo amekuwa Naibu Meya sasa kwa awamu nyingine mfululizo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi huo, Mkuu wa Division ya Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu, Ndg. Pius Sayayi, alisema kwamba Halmashauri ilipokea jina moja la mgombea wa nafasi ya Naibu Meya, hivyo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, jina hilo lilipigiwa kura za "Ndiyo" au "Hapana".
Kwa mujibu wa sheria, mgombea mmoja tu alihitajika kupata asilimia 50 ya kura ili kushinda. Mwenyekiti wa Uchaguzi, Ndg. Said Kitinga, alitangaza matokeo, akisema kwamba Zamda Shabani alishinda kwa kura zote 19 za "Ndiyo", bila kura za "Hapana" wala kura zilizoharibika.
Katika uchaguzi wa kamati za kudumu kwa mwaka 2024/2025, Mhe. Ezekiel Sabo alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Afya, Elimu na Uchumi; Mhe. Hassan Mwendapole alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Madili; na Mhe. Elias Andrea alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji na Mazingira.
Baada ya kutangazwa mshindi, Mhe. Zamda Shabani aliwashukuru madiwani kwa kumuamini tena na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Meya na kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Ndg. Anord Makombe, aliwataka viongozi wote waliochaguliwa kutimiza majukumu yao kwa uaminifu na umoja, akisisitiza kwamba uongozi si suala la bora zaidi bali ni kuonyesha uwezo wa kutekeleza majukumu kwa tija.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464