TAARIFA KWA UMMA
WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA WAKAMATWA
Dar es Salaam, Julai 17, 2024
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inamshikilia SHABAN MUSA ADAM (54) mkazi jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya.
Mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwake Manzese Kilimani tarehe 11 Juni, 2024 akitengeneza dawa za kulevya alizozitambulisha kama heroin kwa kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya akichanganya na kemikali bashirifu.
Baada ya kutengeneza dawa hizo husafirisha kwa kutumia mabasi ya abiria kama vifurushi kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Mtuhumiwa huyo ameieleza Mamlaka kuwa, siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo za kulevya katika nchi za bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya na pia alitumika kama mbebaji wa dawa hizo (punda) na aliporejea hapa nchini aliendelea na uhalifu huo.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya imekamilisha kanzi data (Data base) ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na imeanza uchunguzi juu ya watu hao. Wengi wamebainika wapo ndani ya nchi na wengine nje ya nchi.
Baadhi yao wana biashara nyingine halali lakini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kufanya utakatishaji.
Mamlaka inatoa wito kwao kuachana mara moja na biashara hiyo na kujikita kwenye biashara halali kwani uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Aidha, Mamlaka inamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la MBABA RABINI ISSA mtanzania mwenye pasipoti namba TAE442718, ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior Ndadaye Bujumbura Burundi akiwa na kiasi cha Kilogramu 3.8 za skanka.
Dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwa kushonewa ndani ya begi la nguo. Mtuhumiwa huyo alikamatwa akijiandaa kusafiri kuelekea Dubai.
Kufuatia mikataba ya kikanda na kimataifa iliyosainiwa na Tanzania katika Udhibiti wa dawa za kulevya, mhalifu yeyote wa dawa za kulevya atakaefanya uhalifu katika nchi zilizoingia makubaliano na kukimbilia moja ya nchi hizo atakamatwa.
Vilevile, kupitia ofisi za kanda za Mamlaka zimefanyika operesheni katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Mtwara na Mbeya na kukamata gunia 285 za bangi kavu, kilogram 350 za aina mbalimbali ya dawa za kulevya, milimita 115 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, pamoja na lita 16,523 za kemikali bashirifu zilizokuwa zinasambazwa kinyume cha sheria. Watu 48 wamekamatwa kuhusika na uhalifu huo.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya inathamini na kutambua ushirikikiano unaotolewa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wananchi na Mamlaka nyingine za udhibiti katika kupambana na kudhibiti tatizo la dawa za kulevya nchini.
Imetolewa na,
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.