Mutayoba
Arbogast, Bukoba
WATOTO
wadogo katika Kata ya Kanyigo, wilayani Missenyi mkoa wa Kagera walio chini
ya umri wa miaka nane ambao kwa kiasi kikubwa wanahitaji matunzo anuwai ikiwemo
lishe, wako katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko na yanayoambukiza,
kutokana uhaba wa maji unaosababishwa na kukatika mara kwa mara maji ya bomba
katani humo.
Hali hiyo
imejitokeza wakati tayari serikali ilishaweka miundo mbinu ya maji katika
kata hiyo ya Kanyigo, katika kuhakikisha wananchi hao wanapata maji safi na
salama, ambapo kaya nyingi tayari zimeunganisha maji ya bomba kutoka chanzo cha
maji Omurushenye kupitia tanki la maji Kabambilo.
Bi Ashura
Mohammed, 25 (si jina lake halisi) mwenye mtoto wa umri wa miezi mitatu,
mpangaji katika mtaa wa Kabambilo, kijiji Bugombe katani humo, anaeleza
wasiwasi wake kuhusu mtoto wake anayeharisha, na familia nzima yenye watu sita
kusumbuliwa na tumbo kuwa ni kutokana na kukosa maji bombani na kulazimika
kutumua maji ya chemchemi iliyoko bondeni ambayo kipindi mvua inanyesha,
hutiririsha uchafu hadi chemchemi hiyo.
"Kwa
wiki mbili hatuna maji bombani, na sijui kwa niji tumekatiwa maji ilhali
hatuna deni.Unamuona mtoto wangu huyu jinsi alivyodhoofika, nahisi ni kutumia
maji yasiyo safi na salama, hata sisi matumbo yanauma", alisema mama huyo
Wakazi wa
eneo hilo wamekuwa kuwa wakitafuta njia mbali mbali mbadala kupata maji kwani
wastani wa upatikanaji wa maji katani humo kwa mwezi ni kati ya siku 10 hadi 15
tu.
Familia
zinalazimika kutumia maji kutoka kwenye vyanzo visivyo salama ambavyo vina
kiwango kikubwa cha chumvi au vimechafuliwa,na hivyo kutishia ustawi wao, hasa
watoto wadogo.
Kwa mujibu
wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kata hiyo ilihesabiwa kuwa na wakazi
9,547 kati ya wakazi 245,394 wa wilaya ya Missenyi huku wilaya ikiwa na
watoto 70,090 wa miaka 0 hadi tisa kwa mujibu wa sensa hiyo.
Maji ni
muhimu kwa shughuli za binadamu hususan kwenye kaya kwani hutumika kwa usafi wa
mazingira, utayarishaji wa chakula, bila kuacha usafi wa mwili, huku kaya zenye
Watoto watogo zina uhitaji mkubwa zaidi wa maji.
Taarifa ya
Shirika la Umoja wa mataifa linalohusiana na watoto ulimwenguni(UNICEF)
katika kuadhimisha Siku ya maji Ulimwenguni tarehe 22 Machi 2024, ilisema
watoto zaidi ya 1000 chini ya miaka 5 hufa kila siku kutokana na magonjwa
yanayohusiana na maji.
Mradi wa
miundo mbinu ya maji katika kata hiyo ya Kanyigo, uligharimu shilingi
milioni 684 na ulizinduliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa maji, ambaye sasa ni
Waziri wa maji Jumaa Aweso, Agosti 2020.
Hata hivyo
mradi huo wenye wateja wa maji 645 umeendelea kusuasua kwa kile kinachoelezwa
kuwa ni taratibu zisizoridhisha za kiutendaji, ikiwemo kutumia siku kadhaa
kupata pesa ya LUKU toka Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini, RUWASA,
ambapo kwa mujibu wa mtaalam ambaye hakupenda kunukuliwa
anabainisha kuwa malipo ya madeni ya maji yanaingia katika mfumo wa GePG
(Government electronic Payment Gateway ) ambapo makusanyo yote lazima yaende
Benki kuu (BOT) kwanza kisha kurejeshwa kwa ajili ya matumizi. Hii ni mojawapo
ya sababu ya kuchelewa sana kupata pesa ya LUKU, na kushauri kuwa pawepo
utaratibu wa kuwa na akiba ya fedha ya LUKU wakati wa kusubiria mgao toka
Benki kuu.
Mhasibu wa
mradi wa maji Kanyigo anasema shida kubwa anayokumbana nayo ni idadi kubwa ya
watumiaji maji kushindwa kulipa madeni yao kwa wakati kiasi kwamba kuna wakati
madeni yanakaribia nusu ya matarajio ya ukusanyaji, na hivyo kufanya uendeshaji
wa mradi kuwa mgumu.
Mambo
mengine wanayolalamikia watumiaji maji ni kukatiwa maji hata kama hudaiwi kisa
wengine hawajalipa madeni yao, madai ya bill za maji kutokuwa na uhalisia,
lakini kubwa zaidi ni kuvunjwa kwa Kamati ya maji ya mradi huo bila ufafanuzi
wa kina kwa watumiaji na badala yake kuundwa Kamati nyingine inayoshirikisha
kata jirani ya Kashenye ambayo iko mwambao wa ziwa Victoria na hapo kuna mradi
mkubwa wa kuvuta maji toka ziwani, mradi ambao hata haujaanza kutoa maji
Wananchi
washangazwa na Kamati mpya ya maji inayoongozwa na viongozi ambao wengi wao na
hawapo eneo la mradi huo wa Kanyigo.
Katika hali
isiyo ya kawaida, baada ya mchakato wa serikali kuanza kujenga miundo mbinu ya
kuvuta maji toka ziwa Victoria, mradi uliotambulishwa katani Kashenye
tarehe 7 Julai 2023, RUWASA wilaya ya Missenyi walivunja kiaina Kamati ya maji
Kata ya Kanyigo bila kuwashirikisha watumiaji maji.
Kwa mujibu
wa Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini, (RUWASA) wilaya ya
Missenyi, Mhandisi Andrew Kilembe, mradi huo wa kuvuta maji toka ziwa Victoria
una na thamani ya sh bilioni 1.8, ukitarajiwa kuhudumia kata za Kanyigo,
Kashenye na Bwanjai, na ukikamilika utawafikia wananchi wapatao 23,319
Inaelezwa
kuwa RUWASA wilaya ya Missenyi walivunja kiaina Kamati ya maji Kata ya Kanyigo
bila kuwashirikisha watumiaji maji, na kuunda Kamati moja ya kata hizo mbili.
Mmoja wa wakereketwa wa maji wa kata
Kanyigo Yesse Mushumbusi Kassano anasema, “Hiki kinachoitwa kutuunganisha
kamati za maji za Kanyigo na Kashenye, kuna kosa kubwa sana,aidha kwa kutojua
au makusudi; Kamati ya Kanyigo: ilikuwa na: maji, watumiaji (wadau),
wafanyakazi (watendaji), mapato na miundo mbinu iliyoifanya kufuzu kusajiliwa
kuwa Watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO). Kuiunganisha na eneo lolote
lisilokuwa na vigezo kama hivyo lililonavyo Kanyigo, haikubaliki.” |