Picha hii kwa hisani ya Mtandao, Mtaalamu wa Afya akimfariji mzazi.
Na Salum Maige,Geita
SHIJA Erasto mkazi wa kijiji cha Kikumba Itale wilayani Chato mkoani Geita amedai uzembe wa watoa huduma kwenye zahanati ya Kigongo umesababisha kifo cha mwanae aliyefariki dunia dakika chache baada ya kuzaliwa katika zahanati hiyo.
Akizungumzia hali hiyo Shija amesema, julai 10,mwaka huu majira ya saa 2 usiku alifika kwenye zahanati hiyo akitokwa na damu nyingi kabla ya saa 8 usiku alipoanza kuhangika kujifungua pekee yake huku mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Cesilia Katoba akiwa amelala.
Shija anasema, mara ya kwanza alienda kwenye hiyo zahanati saa 3 asubuhi akitokwa damu ndipo alipewa huduma ya kuzuia damu kutoka na ilivyofika saa 10 jioni aliruhusiwa kurudi nyumbani.
“Asubuhi nikiwa nyumbani, nilianza kutokwa na damu siku ndipo nikamwambia mme wangu anipeleke hospitali na tulipofika damu ikiwa inatoka, niliambiwa na mganga nifanye mazoezi,baadae damu ilikata na ilivyokata kama kwenye saa 10 jioni akaniruhusu nirudi nyumbani” anasema Shija.
Akiwa nyumbani ilipofika saa 2 usiku ile hali ya kutokwa na damu ilijirudia tena, na hivyo akarejeshwa tena kwenye zahanati kisha kupewa kitanda na baadae alitundikiwa dripu ya uchungu.
“Nilifika nikiwa nimeambataa na mama yangu mdogo na dada yangu, nikiwa wodini ndugu zangu hao walifukuzwa wodini na kubaki pekee yangu lakini walikuwa wanakuja wananichungulia huku mganga akiwa amelala” anasema na kuongeza.
“Baadaye saa nane usiku nilihisi uchungu ndipo nilimwita dada yangu ili akamwamshe mganga,mganga alipofika akakuta nipo kwenye hali ya kusukuma na mtoto alikuwa ameshaanza kutoa kichwa, cha ajabu akawa ananiambia unawekaje mguu dirishani,huku nikihisi mwili kuchoka muda mfupi mtoto alitoka na kudondoka kitandani”
Shida anadi kwamba, wakati anahangaika hivyo mganga huyo hakuwa amevaa grovis na baada ya mtoto kutoka akiwa amefunikwa na chupa ya maji mganga alienda kuvaa grovis kitendo kilichosababisha mtoto kunywa maji.
“Ametoka kuvaa grovis anakuja kumtolea chupa mtoto alitoa sauti mara moja tu na hakurudia tena, hata lile kondo hakunisaidia nilisaidia na dada yangu, yeye akihangaika kumpigapiga mtoto lakinui tayari mwanangu alikuwa amefariki dunia” anasema Shija.
Ndugu wa Shija, Kulwa Erasto aliyekuwa ameambatana na mzazi huyo anasema walipofika ndugu yake aliingizwa wodini na yeye kutakiwa kuondoka ndani hadi muda wa usiku wa manane alipoanza kusikia kelele za dada yake kuomba msaada.
Anasema alivyoenda kumuona aliniomba nimwitie mganga ambaye alifika na kuanza kusema maneno yasiyokuwa na staha “akawa anasema tatizo ndugu yenu anakiburi hivi unaweza kujifungua hivi kweli namwambia alale ubavu hataki”
“Hivi kaka mtu anaweza kujifungua kwa kulala ubavu, na hata ile kumsaidia kondo la nyuma litoke hakufanya badala yake mimi ndiye nilihangaika kumbinya tumbo hadi kondo likatoka, kwa kweli huduma haikuwa nzuri toka asubuhi hadi usiku anajifungua” anasema Kulwa.
Mme wa Shija,Austine Warioba anadai kwamba, yeye aliomba kupewa rufaa ya kumpeleka mkewe kwenda kwenye kituo cha Afya au hospitali Chato lakini alikataliwa kwa kuelezwa kuwa gharama za kwenda huko asingeweza kuzimudu.
“Mke wangu kwa hali aliyokuwa nayo niliona kabisa anastahili kwenda hospitali kubwa lakini nilikataliwa, na nilivyotoka pale nikawaacha ndugu zangu wakaanza kuambiwa na mganga kwamba tatizo ndugu yenu mbishi hajiongezi,haya mazingira ya kuambiwa sijiongezi yalikuwa yanaashiria nini” alihoji Warioba.
Warioba anasema, chanzo cha kifo cha mwanae ni uzembe mkubwa uliofanywa na mganga mfawidhi aliyekuwa zamu siku hiyo.
“Yaani basi ilikuwa hata mama wa mtoto tungempoteza wasingekuwa ndugu zangu,lakini niseme tu chanzo cha kifo cha mwanangu ni uzembe mkubwa uliofanywa na mganga kwa sababu alitumia muda mwingi kuvaa grovisi badala ya kumhudumia mtoto sekunde chache baada ya kuzaliwa” aliongeza Warioba.
Mganga mfawidhi wa zahanati ya Kigongo Cesilia Katoba alivyotafuta hakuwa tayari kuzungumza tukio hilo badala yake alimtaka mwandishi wa habari hizi kuzitafuta mamlaka zingine zenye uwezo wa kuzungumzia suala hilo.
Mganga mkuu wilaya ya Chato,Dkt.Eugen Retaisire alipotafutwa kuzungumzia mkasa huo alisema hana taarifa na kuahidi kufuatilia kabla ya kulitolea uafafanuzi jambo hilo.
“Suala la kutokwa na damu ni kawaida si kwamba kila anayetokwa na damu ni kumrifaa, na huwezi kumrifaa mama akiwa anatokwa na damu,lakini nikuahidi ngoja nafuatilia”anasema Dkt. Retaisire.
Hivi karibuni baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliwahi kulalamikia lugha chafu zinazotolewa na na baadhi ya watoa huduma wa zahanati hiyo yakiwemo malalamiko ya kuwatoza hela wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ambao huduma kwao hutolewa bure.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omar Sukari inaonyesha kwamba takwimu za miaka mitatu nyuma, mwaka 2021 kina mama 63 walipoteza maisha ,mwaka 2022 akina mama 57 walipoteza maisha na mwaka jana 2023 akina mama 55 na mwaka huu wa 2024 kuanzia januari hadi mei akina mama 24 walipoteza maisha kabla,wakati na baada ya kujifungua.
Kwa upande wa watoto, mwaka 2022 vifo vilikuwa 905,mwaka 2023 vifo 817 na mwaka huu kipindi cha kuanzia januari hadi mei watoto wachanga 337 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushindwa kupumua, kuzaliwa na uzito pungufu isivyo kawaida.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464