Moja ya Mhudumu wa Afya akimfariji Mgonjwa.
Salum Maige, Geita
MGANGA mfawidhi wa Zahanati ya Kigongo iliyopo kijiji cha Kikumba Itale wilayani Chato mkoani Geita,Cesilia Katoba anayedaiwa na mama mzazi Shija Erasto kusababisha kifo cha mwanae dakika chache baada ya kujifungua haonekani kwenye kituo chake cha kazi.
Inadaiwa kuwa mtumishi huyo hajaonekana kwenye kituo chake cha kazi tangu Julai 20,mwaka huu baada tu ya mwandishi wa habari hii,kuripoti habari inayohusiana na mkasa huo uliotokea Julai 10,mwaka huu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii, inadaiwa kwamba mtumishi huyo amesimamishwa kazi kwa muda kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo za uzembe kazini zilizosababisha kifo cha mtoto mchanga muda mfupi baada ya kuzaliwa.
“Tangu jumapili hajaonekana kazini ,ile tu habari ilivyotoka hatujamuona tena ,inasemekana amesimamishwa kupisha uchunguzi, maana angekuwa amehamishwa tungefahamu” kilisema chanzo hicho.
Aidha, mganga mkuu wilaya ya Chato Dkt. Eugen Retaisire alipotafutwa kuzungumzia hilo hakusema kama amesimamishwa kazi au amehamishwa badala yake amedai yawezekana yuko nje ya kituo chake cha kazi kwa likizo.
“Sijafuatilia sana ,lakini kama haonekani kazini anaweza kuwa yuko likizo”, anasema Dkt.Retaisire.
Kuhusu tuhuma zinazomkabili mtumishi huyo Dkt. Retaisire amesema, suala hilo linafuatiliwa kitaluuma kupitia vyama vya wana taaluma na ikithibitika hatua zitachukuliwa za kitaaluma.
“Sasa hilo suala kuna jinsi ambavyo huwa linashughulikiwa kwani ni professional negligence(uzembe wa kitaaluma),sasa kwa sababu kuna vyama vya wana taaluma, maana yake kama ni kweli anaadhibiwa kitaaluma na ikithibitika hatua zitachukuliwa za kitaaluma” amesema Dkt. Retaisire.
Dkt.Retaisire ameongeza kuwa, kuna timu zinafuatilia mazingira ya tukio hilo yalikuweje kwa sababu lazima wafuatilie wahoji wahusika wakiwemo ndugu wa karibu na watumishi waliokuwepo kazini siku hiyo ya tukio.
“Kama kuna ndugu walikuwepo karibu ,kama kuna watumishi walikuwepo wengine watahojiwa, mwisho wa siku inatoka ripoti ya kiofisi” ameeleza Dkt. Retaisire.
Hivi karibuni Shija Erasto mkazi wa kijiji cha Kikumba Itale wilayani humo alidai uzembe wa watoa huduma kwenye zahanati hiyo ulisababisha kifo cha mwanae aliyefariki dunia dakika chache baada ya kuzaliwa.
Shija alisema, julai 10,mwaka huu majira ya saa 2 usiku alifika kwenye zahanati hiyo akitokwa na damu nyingi kabla ya saa 8 usiku alipoanza kuhangika kujifungua pekee yake huku mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Cesilia Katoba akiwa amelala.
Shija anasema mara ya kwanza alienda kwenye zahanati hiyo saa 3 asubuhi akiwa anatokwa damu nyingi hivyo alipewa huduma ya kuzuia damu kutoka na ilivyofika saa 10 jioni aliruhusiwa kurudi nyumbani.
“Asubuhi nikiwa nyumbani saa 2 damu ilianza kutoka ndipo nikamwambia mme wangu anipeleke hospitali na tulipofika damu ikiwa inatoka, niliambiwa na mganga nifanye mazoezi,baadae damu ilikata na ilivyokata kama kwenye saa 10 jioni akaniruhusu nirudi nyumbani” alisema Shija.
Akiwa nyumbani ilipofika saa 2 usiku ile hali ya kutokwa na damu ilijirudia tena, na hivyo akarejeshwa tena kwenye zahanati kisha kupewa kitanda na baadae alitundikiwa dripu ya uchungu.
“Nilifika nikiwa nimeambataa na mama yangu mdogo na dada yangu, nikiwa wodini ndugu zangu hao walifukuzwa wodini na kubaki pekee yangu lakini walikuwa wanakuja wananichungulia huku mganga akiwa amelala” alisema na kuongeza.
“Baadaye saa nane usiku nilihisi uchungu ndipo nilimwita dada yangu ili akamwamshe mganga, mganga alipofika akakuta nipo kwenye hali ya kusukuma na mtoto alikuwa ameshatoa kichwa, cha ajabu akawa ananiambia unawekaje mguu dirishani,huku nikihisi mwili kuchoka muda mfupi mtoto alitoka na kudondoka kitandani”
Shida anadai kwamba, wakati anahangaika hivyo mganga huyo hakuwa amevaa grovis na baada ya mtoto kutoka akiwa amefunikwa na na ile chupa ya maji mganga alienda kuvaa grovis kitendo kilichosababisha mtoto kunywa maji hayo ambayo ni machafu.
Mme wa Shija,Austine Warioba anadai kwamba, kutokana hali ya mkewe ya kutokwa na damu nyingi aliomba kupewa rufaa ili kumpeleka kwenye kituo cha Afya au hospitali Chato lakini alikataliwa kwa kuelezwa kuwa hana uwezo wa kumudu gharama za kwenda huko.
“Yaani basi ilikuwa hata mama wa mtoto tungempoteza wasingekuwa ndugu zangu, lakini niseme tu chanzo cha kifo cha mwanangu ni uzembe mkubwa uliofanywa na mganga kwa sababu alitumia muda mwingi kuvaa grovisi badala ya kumhudumia mtoto sekunde chache baada ya kuzaliwa” anasema Warioba.
Hata hivyo,mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Cesilia Katoba alivyotafuta hakuwa tayari kuzungumza tukio hilo badala yake alimtaka mwandishi wa habari hizi kuzitafuta mamlaka zingine zenye uwezo wa kuzungumzia suala hilo.
Hivi karibuni baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walimlalamikia mtumishi huyo kwa lugha chafu kwa wateja wake wakiwemo wajawazito na wale wanaochelewa kupeleka wagonjwa ambao walidai kutozwa fedha hata huduma zinazotolewa bure.
Baadhi ya wananchi wa Kikumba Itale walisema, mganga mfawidhi wa zahanati hiyo ameendekeza migogoro, kutumia lugha chafu kwa wagonjwa hasa wanapofika kupata huduma wakiwa katika hali mbaya.
Yasinta Petro ni miongoni mwa wananchi walioonja machungu ya hali hiyo baada ya kupeleka mwanae wa mwaka mmoja katika zahanati hiyo akiwa na hali mbaya na alivyofika alifukuzwa kwa sababu ya kusahau kadi ya kliniki ya mtoto nyumbani.
“Sasa ,hivi ugonjwa huwa unakuja na hodi?, badala ya mtoto kumhudumia unaulizwa maswali yasiyokuwa na msingi, tunatukanwa, tunakaripiwa, huduma ni mbovu sana, hatuoni umuhimu wa hii zahanati”
Musimu Maneno mkazi wa kitongoji cha Mwaloni ilipo zahanati hiyo alisema, tangu mganga huyo afike katika kituo hicho huduma za matibabu zimekuwa mbaya.
Alisema, mbali na kutumia lugha chafu baadhi ya akina wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hutozwa faini ya shilingi 3,200 ilihali serikali inasema huduma kwao ni bure.
Mkazi mwingine anayefahamika kwa jina la Plakseda John alisema, kuna wakati wanakosa dawa katika zahanati hiyo licha ya kutakiwa kutoa fedha kiasi cha sh.3,200 kwa ajili ya matibabu ya watoto.
“Kuna umuhimu gani sasa, unaenda unatozwa fedha, serikali inasema huduma ni bure kwetu sisi wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, ukishatoa hela unaambulia panado zingine unaambiwa ukanunue sasa dawa zinazoletwa na serikali zinaenda wapi?”, amehoji Plakseda.
Diwani wa kata ya Kigongo Mashaka Mchezela alipouliza kuhusu malalamiko ya wananchi hao,alihusisha na masuala ya kisiasa hasa katika kuelekea kwenye uchaguzi ukiwemo wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani ambapo alidai kuna makundi yanaendekeza chuki ili kuwachafua viongozi walioko madarakani.
Usalama na uhai wa watoto kabla,wakati na baada ya kujifungua umekuwa ukiwekwa njia panda kutokana na huduma duni zinazotolewa na baadhi ya watalaamu wa afya, mazingira yasiyo rafiki kati ya watoa huduma na wataalamu wa afya kwenye baadhi ya vituo vya Afya nchini
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omar Sukari inaonyesha kuwa, takwimu za miaka mitatu nyuma, mwaka 2021 kina mama 63 walipoteza maisha ,mwaka 2022 akina mama 57 walipoteza maisha na mwaka jana 2023 akina mama 55 na mwaka huu wa 2024 kuanzia januari hadi mei akina mama 24 walipoteza maisha kabla,wakati na baada ya kujifungua.
Kwa upande wa watoto, mwaka 2022 vifo vilikuwa 905,mwaka 2023 vifo 817 na mwaka huu kipindi cha kuanzia januari hadi mei watoto wachanga 337 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushindwa kupumua, kuzaliwa na uzito pungufu isivyo kawaida.
Sababu zingine za vifo hivyo ni uzazi pingamizi ,kuchelewa kufika kwenye huduma za Afya ,kutokwa na damu nyingi kabla, wakati na baada ya kujifungua.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464