Header Ads Widget

MILIONI NNE YATENGWA KATIKA UTOAJI WA ELIMU YA LISHE REDIONI


Wataalamu wa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama wakipokea PJT-MMMAM baada ya kzuinduliwa

Na Kareny Masasy

HALMASHAURI  ya  Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga  baada ya kuzindua programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  (PJT-MMMAM)  Mwezi Februari mwaka huu imeamua kutenga bajeti ya shilingi Milioni nne kwaajili ya uelimishaji masuala ya lishe kupitia vyombo vya habari.

Ofisa mipango wa halmashauri hiyo Mhoja  Shigela anasema Bajeti hiyo ilipitishwa kwenye kikao cha baraza la madiwani  kwa Mwaka wa fedha wa 2024/2025 kuwa  zitatumika katika utoaji wa elimu ili  kuwafikia wananchi.

“Elimu ya  Lishe imekuwa ikitolewa na   wahudumu wa Afya  ngazi ya jamii  ambapo  wamesaidia  uhamasishaji kwa wajawazito kuhakikisha wanafuata taratibu za lishe  ili kuepuka kuzaa watoto wenye changamoto za aina mbalimbali”anasema Shigela.

Shigela anasema  bado vyombo vya habari upande wa Redio utatumika kusaidia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ambao wanashindwa kufika kwenye maeneo yaliyopembezoni zaidi kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara na jiografia ya eneo husika.

Wakazi wa kijiji cha Kundihili kata ya Ukune halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga   Sesilia James  na Bernadetha  Elias  wenye ujauzito wanasema elimu ya lishe wakati mwingine wamekuwa wakiisikiliza  kwenye vyombo vya habari.

 Mwenyekiti wa kijiji hicho Makungu Shilunga anasema wenye watoto na wajawazito wanahimizwa kwenda kliniki na wataalamu wa afya  licha ya kutolewa elimu wamekuwa wakisikiliza kwenye vyombo vya habari

Mtendaji wa kijiji cha Kundihili  Neema Chacha anasema zoezi la utolewaji wa elimu ya lishe limekuwepo kwa kushirikiana na wahudumu ngazi ya jamii ambapo kila robo ya mwaka  wanatoa elimu ya lishe kupitia mkutano wa hadhara nakuelezwa wasikilize sana elimu kupitia redio  wasipende maigizo na miziki pekee.

 “Kijiji hiki kina kaya 349  na  wakazi  1574 ambapo  mpaka sasa hakuna takwimu ya mama aliyezaa mtoto mweye tatizo la mgongo wazi au kichwa kikubwa kama wapo basi takwimu hiyo ya zamani hata umri wao ni mkubwa kuanzi miaka 10”anasema Chacha.

Ofisa lishe kutoka halmashauri ya Ushetu Hadija Nasibu  anasema  wapo wananchi wanaosikiliza redio endapo itatolewa elimu ya umuhimu wa Folic Acid  mama  aliye na changamoto hiyo akisikia atachukua hatua.

“Tunajitahidi kutoa elimu kwenye jamii kwa kushirikiana na wahudumu ngazi ya jamii kuanzia kwenye vitongozji  kwa kuwasaka wajawazito kuwapa elimu ya umuhimu wa lishe na sasa watatumia redio  kuandaa vipindi japo mara moja mbili kwa wiki”anasema Nasibu.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Ushetu  dk Othman  Matindo anasema kuna wahudumu wa afya ngazi ya jamii zaidi ya 5000 ambao jukumu lao kupita kila kaya yenye watoto na wajawazito kutoa elimu ikiwemo suala la lishe.

“Kama redio nazo zikifikisha ujumbe zitasaidia kuhakikisha wananchi wanapata elimu  ya umuhimu wa lishe nakuondoa changamozto zitakazojitokeza”anasema  Dk Matindo.

 Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema  wapo baadhi ya wajawazito kuwa na tabia ya kufuata mtindo wa maisha wa ulaji  wa kutofuata makundi matano ya  vyakula ambayo ndiyo kichocheo cha kuongeza madini ya Folic acid mwilini.

“Sasa tunawasisitiza wafuatilie vyombo vya habari katika maeneo yao kwani elimu  sasa imekuwa ikitolewa  wanapokwenda kliniki wanakuwa tayari wanaongezea uelewa”anasema  Hamis.

Ofisa habari  na mawasiliano  kutoka shirika la Child Help Tanzania  Milton Byemerwa anasema madini ya foliki acidi  ni madini yatokanayo  kwenye vyakula vitokanavyo na wanyama kama vile Maziwa, mayai,nyama na samaki na vyakula vya mbogamboga  na matunda.

Byemerwa  anasema mama akikosa madini hayo mwilini anao uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto mwenye ulemavu  wa mgongo wazi na kichwa kikubwa.

Byemerwa  anasema kila mzazi anatamani kuzaa mtoto akiwa na afya njema  lakini tatizo linakuja  mama anapokuwa mjamzito anakosa madini ya foliki acidi.

Byemerwa  anasema  upatikanaji wa vyakula hivyo ni rahisi siyo gharama mama anatakiwa ale  kipindi chote cha  ujauzito na njia nyingine anashauriwa ameze vidonge vyenye madini ya foliki acid  miezi mitatu kabla ya kupata ujauzito.

“Madhara yatokanayo na ukosefu wa viini lishe mwilini  kwa mjamzito anapobahatika kupata mtoto  ndipo linajitokeza tatizo la mgongo wazi,  hutokea kwenye paji la uso,utosini, uti wa mgongo, na kichwa kikubwa”anasema Byemerwa.

Byemerwa anasema   ubongo wa mtoto na mishiba ya fahamu inatengenezwa ndani ya wiki tatu  tangu kutungwa kwa mimba na mama akiwa hana madini ya kutosha mwilini changamoto hujitokeza kwa mtoto anayezaliwa ikiwemo ulemavu.

Byemerwa  anasema wanachokifanya  sasa hivi  kwa watoto wanaozaliwa  ulemavu huo ni kuwatafutia tiba  na kuwaunganisha na madaktari bingwa pamoja na chama cha wazazi wenye watoto wa aina hiyo.

Hapa Tanzania  kwa mujibu  wa  Waziri wa afya Ummy Mwalimu  mwaka jana amesema  watoto zaidi ya   6000 kila mwaka wanazaliwa na tatizo la ulemavu wa aina hiyo.

 “Hapa duniani  vizazi hai  1000  ikiwa wastani watoto  watatu mpaka wanne wanazaliwa na mgongo wazi na  kichwa kikubwa changamoto kubwa ni ukosefu wa lishe kwa mama kabla ya kupata ujauzito”anasema  waziri Ummy.

Ofisa lishe kutoka taasisi ya chakula na lishe nchini (TFNC) Doris Katana anasema Uongezaji virutubishi  maana yake ni kiwango cha kuongeza vitamin au virutubishi kwenye vyakula vya kawaida vinavyopatikana kwenye jamii.

“Lengo kubwa  ni kuboresha hali ya mlaji kwa nia ya  kuzuia na kutibu matatizo ya virutubishi mwilini  hasa  kwa kuanza na  vijana balehe”anasema Katana .

Katana anasema virutubishi hivyo ni madini chuma, vitamin A,  Madini joto lengo kuzuia pale tatizo linapotokea  mfano watu wamekuwa wakitumia mtindo wa maisha  kwenye vyakula vingi ambavyo havina madini.

“Madini ya foliki acidi    ni muhimu kwa mama mwenye umri wa kuzaa  akiwa na upungufu  wa madini hayo hitilafu inatokea na ndipo anampata mtoto mwenye ulemavu huo”Katana .

Katana anasema   ili mama aweze kukaa vizuri hali ya mwili wake wa kujiandaa kupata mtoto  anahitaji  madini hayo yenye  macrogramu 400 kila siku ale matunda,mbogamboga, jamii ya mikunde mayai kwa wingi  nakushauriwa kutumia vidonge vya foliki acidi.

Katika kukabiliana na tatizo la udumavu  nchini waziri mkuu Kassimu Majaliwa amesema serikali inatarajia kutenga  bajeti kwaajili ya ununuzi na usambazaji wa  mashine  maalum za kuchanganya virutubisho kwenye vyakula.

MWISHO..

 

Post a Comment

0 Comments