MKUU WA WILAYA YA MTWARA ATEMBELEA VISIMA VYA GESI NTORYA 1 NA 2, KATA YA NANGURUWE


Meneja Mradi wa gesi asilia-Ntorya Patrick Kabwe akifafanua jambo kwa Mhe.Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda alipotembelea kisima cha gesi -Ntorya 1

***
Julai 6,2024

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Mwanahamisi Munkunda amefanya ziara ya kutembelea visima vya gesi asilia (Ntorya-1 na kisima cha Ntorya 2) katika kata ya Nanguruwe ili kujionea maendeleo ya visima hivyo.

Meneja mradi Patrick Kabwe alieleza kuwa licha ya maendeleo ambayo yamefanyika katika visima hivyo viwili, TPDC na kampuni ya ARA wanakusudia kuchimba kisima cha tatu cha Chikumbi-1 ili kuongeza uzalishaji wa gesi asilia.

‘‘Sasa hivi tunakusudia kuanza uzalishaji wa gesi asilia kwa awamu , awamu ya kwanza ya uzalishaji tunategemea kuanza mwezi Aprili, 2025, pamoja na hayo kutakuwa na uchorongaji wa kisima cha Chikumbi-1 katika kijiji cha Namahyakata barabarani ambapo visima vyote vitatu (03) vikiwa kwenye uzalishaji vitazalisha hadi futi za ujazo milioni 60 kwa siku’’, amesema Kabwe.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya amepongeza uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuwa thabiti kwenye shughuli za utafutaji na uendelezaji wa nishati ya gesi asilia pamoja na kuwa wa mfano kwenye utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii ‘CSR’ mkoani Mtwara.

"Nawapongeza sana TPDC kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya gesi mkoani Mtwara, kwetu sisi ni fursa kwani wananchi wanapata ajira, kuongeza pato la halmashauri kupitia Mrabaha pamoja na uboreshwaji wa huduma za kijamii kupitia CSR mfano mzuri ni ujenzi wa kituo cha Afya cha Msimbati",ameongea Mkuu wa Wilaya.

Ziara hiyo imeambatana na Maafisa kutoka TPDC, ARA Petroleum, APY-KEGS Energy pamoja na Kamanda wa Polisi wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya akiwa katika ziara kisi ma cha Ntorya-2 , Kata ya Nanguruwe

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amefanya kikao na wananchi wa Kata ya Nanguruwe kwa lengo la kuhamasiha ushiriki wao kwenye mradi, kikao hicho kimehudhuriwa na maafisa wa TPDC, ARA Petroleum na kampuni ya APY-KEGS Energy pamoja na viongozi kutoka ngazi ya Wilaya.

"Nitoe rai kwa wananchi wa Kata ya Nanguruwe kuwapokea wawekezaji pamoja na kutoa ushirikiano utakaohitajika",ameongeza Mhe. Mkuu wa Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mh.e Mwanahamisi Munkunda akiongea na wananchi wa Nanguruwe
Wananchi wa Nanguruwe wakifuatilia mkutano

Vilevile, Mhe Mwanahamisi ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita (6) ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwenye sekta ya gesi asilia mkoani Mtwara hali inayoinua chachu ya maendeleo mkoani humo.

#TPDCTUNAWEZESHA
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464