WANANCHI WALILIA SHULE SHIKIZI IFUNGULIWE KUWANUSURU WANAFUNZI ELIMU YA AWALI KUTEMBEA UMBALI MREFU



https://mail.google.com/mail/u/0/images/cleardot.gifWanafunzi wa darasa la Awali mkoani Geita

Salum Maige, Geita

Mwaka 2024 mkoa wa Geitab ulijiwekea malengo ya kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali 108,385 lakini hadi zoezi la uandikishaji likamilike mwezi machi 31,mwaka huu mkoa huo ulikuwa haujafanikiwa baada ya kuandikisha wanafunzi 84,609, wavulana 41,983 na waschana 42,625 sawa na asilimia 78,

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya idara ya elimu iliyotolewa na katibu tawala anayeshughulikia elimu Antony Mtweve wakati akizungumzia taarifa ya uandikishaji wa darasa la awali na darasa la kwanza mwaka 2024.

Baadhi ya sababu zinazotajwa  kutofikia lengo hilo ni umri mdogo wa watoto wanaopaswa kuanza darasa la awali ukilinganisha na umbali wa kutoka nyumbani kwenda shule ziliko.

Afisa elimu taaluma mkoa wa Geita Cassian Luoga anakiri kuwepo kwa hali hiyo na kubainisha sababu zingine kuwa ni mito kujaa maji, hivyo watoto hushindwa kuvuka wakihofia kusombwa na maji na wakati mwingine wazazi kutotambua umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto wao.

“Umbali kutoka kwenye majumba yao kwenda shule zilizopo inakuwa ni ngumu sana ukilinganisha umri wao,lakini tunawapa elimu wazazi walau kuwasindikiza watoto kwenda shule na kuwafuata ili tu wapate haki yao ya elimu ya awali ambayo ndiyo msingi wa elimu”, alisema Luoga.

Mwandishi wa Makala haya, anasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 30 kutoka Geita mjini kufika kijiji cha Ibisabageni hadi kitongoji cha Kabulabunyasi ambako kwa mbali kunaonekana majengo ya madarasa mawili yakiwa yamezingirwa na nyasi ndefu.

Katika kuyasogelea majengo hayo yanaonekana kuanza kuchakaa kwani yana muda mrefu toka yakamilike kujengwa hayajaanza kutumika hivyo kugeuka makazi ya viumbe wengine kama popo, na wadudu wengine wadogo wakiwemo buibui.

Nilivyozungumza na wananchi wa kitongoji hicho wanadai madarasa hayo yana zaidi ya miaka mitatu toka yakamilike na yalijengwa kwa lengo la watoto wa awali,la kwanza na la pili waweze kusomea karibu ili kuwapunguzia umbali wa kutoka na kwenda kusoma katika shule ya msingi Ibisabageni umbali wa zaidi ya kilomita saba.

Wananchi hao wamefanikiwa kujenga vyumba viliwi vya madarasa, ofisi ya walimu na vyoo vya wanafunzi, lakini tangu wakamilishe ujenzi huo miaka mitatu iliyopita shule hiyo haijafunguliwa jambo ambalo limewakatisha tamaa kuendelea kujenga madarasa mengine.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ibisabageni James Masangwa ni kwamba shule hiyo ilijenga kwa ajili kuwanusuru wanafunzi wanaotoka vitongoji vya Kabulabunyasi na Nyenye ambao hutembea zaidi ya kilomita 14 kutoka na kwenda shule.

Mwenyekiti anasema, kutokana na adha hiyo wananchi walihamasishana kujenga shule hiyo shikizi kwa ajili ya watoto wale wa awali,la kwanza na la pili ambao kutokana na umri wao hushindwa kuhimili safari ndefu ya kufika shule ya msingi Ibisabageni.

“Tulifuatilia serikalini ili shule hiyo ianze, watu wa serikali walisema hawawezi kuruhusu kuanza shule hiyo hadi wananchi wajenge walau wafikishe madarasa manne, ndipo itasajiliwa. Sasa hii imewakatisha tamaa wananchi ,wao walitamani sana waone watoto wanasoma ili waendelee na madarasa mengine” anasema mwenyekiti.

Anasema, kutokana na jografia ya eneo hilo baadhi ya wazazi wa vitongoji hivyo hulazimika kwenda kuwaandikisha watoto wao katika shule ya msingi Busekeseke iliyopo halmashauri ya Buchosa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

“Lakini hii shule ingeanza darasa la awali,la kwanza na la pili ingewahamasisha wananchi kuendelea na ujenzi kwani wanasumbuka watoto wao hasa kipindi cha mvua zinaponyesha ambapo daraja lilishakatika ambapo hushindwa kuvuka” ,anasema Masangwa.

Baadhi ya wazazi wamesema ,kipindi cha mvua zinaponyesha kuna mto watoto hushindwa kuvuka na hivyo hulazimika kuwasubiri watoto wao wakati wa kutoka shule ili kuwavusha.

“Kila siku hasa kipindi cha mvua huwa tunakuja na watoto hadi kwenye mto tunawavusha na kabla ya kutawanyika wazazi huwa tunaenda eneo hilo kuwasubiria ili kuwavusha, tunaiomba sana serikali ituruhusu watoto wetu hawa wadogo waweze kusomea hapa”, anasema Paul Kahindi.

Salome Zacharia anasema, watoto wamekuwa wakishindwa kupita katika daraja ambalo limeshakatika kwenye kipindi cha mvua hujaa maji na hivyo baadhi ya watoto hushindwa kuhudhuria masomo inavyotakiwa kutokana na umbali na hali mto kujaa maji.

“Tunaomba msaada kwa shule yetu iweze kufunguliwa ili watusaidie wazazi, tumejitahidi kujitolea ili tuhamasike, wangeturuhusu hawa watoto wadogo wakawa wanasomea hapa” anasema Salome.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Ibisabageni wanaoishi kwenye vitongoji vya Kabulabunyasi na Nyenye wanasema, wanachoka kutembea umbali mrefu na kuna baadhi hunusurika kwenda na maji wakati wa mvua.

“Kipindi cha mvua hapa huwezi kupita ,wazazi ndiyo hutusaidia kutuvusha,hii hali inatusababishia kuchelewa hata masomo tunakuta wenzetu wako darasani wameanza kusoma, hivyo serikali ingetusaidia tuweze kusomea karibu” anasema mmoja wa watoto wa darasa la pili.

 

Mwnyekiti wa kamati ya shule ya msingi Ibisabageni Steven Pande anasema shule shikizi ya Mkuyuni iliyojengwa na wazazi ingeanza ingesaidia kupungua msongomano wa wanafunzi shuleni hapo.

Anasema, Shule hiyo ina wanafunzi 1,440 idadi ambayo ni kubwa na hivyo wastani wa wanafunzi 300 hutumia darasa moja jambo linalosababisha kuwepo kwa msongamano darasani na hivyo walimu inawawia vigumu kuwafuatilia watoto wote kwa wakati mmoja.

“Mwalimu mmoja anatakiwa kuhudumia watoto 45 kwa darasa moja, lakini kwetu watoto ni wengi mno, na ndiyo maana wananchi waliamua kujenga shule mpya shikizi ili kupunguza msongamano na umbali wa kutembea kwenda na kutoka shule” anasema Pande.

Katika taarifa ya kata ya Isulwabutundwe, diwani wa kata hiyo James Maweda ombi lake kwa serikali ni shule hiyo iweze kufunguliwa ili kupunguza utoro shuleni hasa wakati wa mvua ambapo mito hujaa maji.

“Hii shule ikifunguliwa itapunguza utoro katika shule ya msingi Ibisabageni hasa kipindi cha mvua kwani wanafunzi wa madarasa ya awali la kwanza na pili husindwa kuvuka kwenda shule”, alisema Maweda.

Aidha, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Karia Rajabu Magaro amekiri kuitambua shule hiyo na kueleza kwamba shule shikizi zilizojengwa na wananchi ni nyingi na karibu kila kata ina shule shikizi zaidi ya nne.

Anasema, na shule hizo zimekuwa zikifunguliwa kwa awamu kulingana na madiwani wanavyopitisha bajeti na kwa kutambua umuhimu wa kila mahali kwa kuzingatia bajeti ya serikali ilivyoelekeza.

“Shule ya msingi shikizi ya Mkuyuni inafahamika, na ndiyo maana wakaruhusiwa(wananchi),  kuanza kujenga ,lakini inaweza ikaanza kwa bajeti ya mwaka huu wa fedha 2024/2025.Hivyo nimuombe mwenyekiti aongee na diwani wake tuone tunafanyeje ili shule hiyo ianze kipindi hiki cha bajeti”, anasema Magaro.

Katika mwaka wa masomo wa 2024 halmashauri ya wilaya ya Geita ilitarajia kuandikisha wanafunzi wa darasa la elimu ya awali 38,249 wavulana wakiwa 18,891 na waschana 19,358 lakini haikufikia lengo baada ya kuandikisha wanafunzi 33,183 wavulana 16,421 na waschana 16,762 sawa na asilimia 78.

Shule hiyo ni muhimu kufunguliwa kwa maslahi mapana ya watoto,mbali tu na kupunguza utoro italeta hamasa kwa watoto kupenda kwenda shule kujifunga, kadhalika italeta hamasa kwa wananchi kuchangia nguvu na mali zao kufanya maendeleo, kuchochea uwajibikaji kwa jamii na kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Hivyo serikali inao wajibu wa kuhakikisha shule hiyo inafunguliwa ili kuleta hamasa kwa pande zote za jamii pamoja na kutosababisha kuchakaa kwa majengo yaliyojengwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita bila kutumika.

 

Tanzania ni moja ya nchi za mwanzoni katika ukanda wa Afrika Mashariki kuanza  kuifanya  elimu ya awali kuwa ya lazima kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kujumuisha elimu ya awali katika elimu ya msingi kwa shule zote za msingi kuwa nadarasa la elimu ya awali.

Licha ya sera hiyo kuwa na malengo mahususi zipo baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa darasa la awali ambao kwa mujibu wa sera hiyo wanatakiwa kuanza elimu ya awali wakiwa na umri chini ya miaka mitano.

Katika maeneo mengi hapa nchini Tanzania watoto darasa la awali wanakabiliwa na umbali mrefu wa kutembea zaidi ya kilomita 10 kwa siku kwenda na kutoka shule wanakosoma.

Hali hii imekuwa ikiwaadhiri watoto hao wakiwemo wenzao wa darasa la kwanza na pili ambao umri wao ni mdogo chini ya miaka minane ambao ni kundi lengwa kwenye mpango jumuishi wa taifa la malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na hivyo wazazi wakati mwingine hushindwa kuwaandikisha shule.

Mbali na changamoto hiyo wakiwa njiani, kuna wakati wanakwama kufika shuleni hasa kipindi cha mvua zinaponyesha ambapo baadhi ya njia hujaa maji na hivyo kushindwa kuvuka mito ili kufika kwenye shule wanakosoma.








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464