KUTOKUMEZA DAWA ZA FOLIC ACID KUMESABABISHA ULEMAVU KWA MTOTO

Mtoto   aliyezaliwa na ulemavu

Na Kareny  Masasy,

TATIZO  la mtoto mwenye umri wa miaka mitatu  aliyebainika kuzaliwa na  ulemavu wa kichwa kikubwa na viungo vya mwili kukosa nguvu haja ndogo na kubwa kutoka bila kujua  pamoja na kushindwa kutembea linaweza kutibika wasimuache akaendelea kuteseka.

Daktari bingwa magonjwa ya  watoto  kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk Justina Tizeba anasema  tatizo hilo likiwahiwa linataibika vizuri.

Akitoa ushauri kwa familia yenye mtoto  huyo   dk Tizeba anasema  umri wa mtoto  bado ni mdogo kama  walikosa uwezo wa kufatilia matibabu  kama walivyoelekezwa na wataalamu wajitahidi kufika kwenye ofisi za serikali  kwa mkuu wa wilaya au mkoa ili wapatiwe kibali cha kupata matibabu.

Dk Tizeba anasema  mama anapata ujauzito miezi mitatu  ya mwanzo  kitaalamu ni wakati wa uumbaji  wa mtoto anatakiwa apate vidonge vya Folic Acid  ambavyo vitasaidia kuimarisha uti wa mgongo na mifupa lakini inaonekana mtoto huyo hakupata ipasavyo.

“Ndiyo maana huwa tunashauri  mama anywe folic Acidi miezi mitatu ya mwanzo na baada ya kujifungua siku 42  ili kujenga mifupa na  kusiwepo na matatizo ya mtoto  kuzaliwa na changamoto zozote  na katika ukuaji wake.

Dk Tizeba  anasema Mama asipofuatilia  ushauri wa wataalamu  na kuacha kutumia Folic Acid ipasavyo  upo uwezekano wa mtoto  kuzaliwa kichwa kikubwa,Mgongo wazi au tundu nakushindwa kutembea wakati mwingine kutokwa  haja kubwa au ndogo bila kujijua.

“Mtoto huyo matatizo yote hayo anayo  nakutambaa kwa kurudi kinyume nyume ni uti wa mgongo kukata mawasiliano yameenda kuathiri pia ubongo lakini umri wake bado ni mdogo anatibika wasizebee wazazi kumpeleka kwa wataalam”anasema DK Tizeba.

Dk bingwa wa magonjwa ya  wanawake  kutoka hospitali ya Rufaa ya  Mkoa  wa Shinyanga  Dk Agustino Maufi anasema Mjamzito anatakiwa ahudhurie Kliniki  ili apate maendeleo ya ukuaji wa mtoto wake.

 “Na hivi sasa  serikali imeongeza mahudhurio  kwa wajawazito yalikuwa mahudhurio manne  na sasa yamefika mahudhurio  nane lengo kuhakikisha mtoto anapata maendeleo  mazuri akiwa tumboni na mama kuweka mahusiano mazuri na watoa huduma .”anasema  Dk Maufi.

Dk Maufi anasema  asilimia 57 ya wanawake  wanakutwa na  viashiria vya upungufu wa damu  na changamoto  ya kutoka kwa mimba  au kuzaliwa kwa mtoto amekufa.

Dk Maufi anasema  mjamzito anatakiwa apimwe mara kwa mara  kwa kuhudhuria kliniki ili kuepuka  changamoto hizo na mtoto kuzaliwa akiwa na afya njema.

Mratibu wa afya ya Mama na Mtoto mkoa wa Shinyanga Halima Hamis anasema  mkoa wa Shinyanga una asilimia 34 ya Mahudurio ya kliniki kwa wiki 12 za mwanzo ukilinganisha na kitafifa ni asilimia 60.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema kuwa Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022  jumla ya wanawake wajawazito 1,784,809 walihudhuria Kliniki na kupatiwa huduma za afya.

Waziri Ummy anasema kuwa  asilimia 99.7 ya akinamama wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020, hata hivyo changamoto iliyopo ni wanawake wajawazito kuchelewa kuhudhuria klinik wapatapo ujauzito,” amesema Ummy.

“Takwimu zinaonesha kuwa kati ya wajawazito 1,784,809 ni wajawazito 656,040 sawa na asilimia 37.6 walianza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito ikilinganishwa na asilimia 36 ya kipindi kama hiki mwaka 2020,” ameongeza.

Mtendaji wa kata ya Usule iliyopo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  Shimba Masesa anazungumzia tatizo alilonalo mtoto jina limehidahiwa kuwa alizaliwa na ulemavu wa viungo na kichwa kikubwa.

Masesa anasema tatizo la mtoto huyo ni kuwa hawezi kujihudumia  na hata bibi yake anayeishi naye  hawezi kuondoka kwenda popote na kumuacha.

Hatua niliyochukua nimemwandikia barua ya utambulisho na kuweka taarifa zake za kumbukumbu ofisini ili aweze kupata msaada zaidi.

Masesa anasema mtoto huyo anaongea vizuri na umri wake wake ni miaka mitatu anaweza kwenda  kuanza shule  changamoto hali aliyonayo kumbe inatibika.

Mwenyekiti wa kijiji  cha Igalamya  kata ya Usule Felister  Bundala anasema walianza jitihada za kuwaunganisha na viongozi ikiwemo mkuu wa wilaya  kuhakikisha mtoto huyo anapata msaada wa haraka.

Baba wa mtoto huyo  Samson Saramba anasema  alizaliwa mwaka  2021  katika Zahanati ya kijiji cha Usule na tatizo hilo lilibainika mwaka huo baada ya wauguzi kuona eneo la Mgongo wa mtoto kuna kovu jeusi.

Saramba anasema Kovu hilo lilianza kuongezeka  nakuwa Nundu hali iliyolazimu wamrudishe kwenye Zahanati nakupatiwa rufaa ya kwenda kituo cha Afya Tinde  kilichopo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na wataalamu wa hapo waliwapa rufaa ya kwenda Bugando.

Saramba anasema  alifanyiwa  upasuaji wa mgongo kuuziba  na kushonwa  katika hospitali ya rufaa  Bugando  lakini kichwa kiliendelea kuwa kikubwa na miguu ilizidi kukosa nguvu.

Saramba anasema  walielezwa warundi kliniki Bugando kwaajili ya uangalizi lakini hawakuwahi kurudi tenda kutokana na kukosa fedha za nauli ya kumrudisha  Bugando.

“Ninaweza kuanza kufuatilia  kliniki ya mwanangu tena kwa ushauri nilioupata nitaenda kuonana na viongozi ili nipatiwe huduma bure mimi sina uwezo gharama za usafiri ni shida”anasema Saramba.

Mama wa mtoto huyo  wanadai  mahudhurio ya kliniki yalikuwa sio mazuri kutokana na kutoelewana na mama mkwe wake ikiwemo maisha duni  ndani ya familia.

Serikali   ya Tanzania kupitia  sera ya afya ya mwaka 2007  imewekeza katika kuboresha  uhai wa mtoto kupitia  utoaji wa huduma bure za  afya kwa  wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Taarifa  za utafiti zilizotolewa na TDHS-MIS za mwaka 2015 hadi 2016 zinaonyesha  mafanikio makubwa  ya  asilimia 98.9 hapa nchini  ni mahudhurio ya wajawazito  kliniki waliohudumiwa  na wataalamu wenye ujuzi  kwenye vituo vya afya  kutoka asilimia 96 ya mwaka  2010.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464