TAKUKURU:MGOMBEA MTOA RUSHWA HAWEZI KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI, SEMINA YA WAANDISHI WA HABARI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga, imewatahadharisha wananchi wawe makini katika chaguzi zijazo, kwa kuchagua wagombea wenye sifa na uwezo wa kuwaletea maendeleo na siyo watoa rushwa.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amebainisha hayo leo Agosti 7,2024 katika ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari mkoani humo,inayohusu nafasi ya vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema kuwa ni muhimu kwa waandishi wa habari kutoa elimu kwa wananchi, ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika chaguzi zijazo,ukiwamo wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani 2025.
Kessy alisisitiza kwamba rushwa inatishia demokrasia na inawanyima wananchi haki yao ya kupata viongozi waadilifu.
"Wagombea watoa rushwa hawawezi kuwaletea maendeleo wananchi, na vitendo vya rushwa vinaweza kuondoa nafasi za wagombea wenye sifa,"amesema Kessy.
“Wananchi wanapaswa kuwa na ufahamu wa kutosha ili waweze kufanya maamuzi sahihi na kuchagua viongozi wanaofaa,”ameongeza Kessy.
Pia,amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili katika kazi zao na kuepuka kutumiwa na baadhi ya wanasiasa, ambao wanajaribu kuwapatia rushwa ili kuandika habari zinazompamba mgombea asiyefaa au kumchafua mwingine.
Naye Mkuu wa dawati la elimu kwa umma kutoka Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mohamed Doo, akizungumza wakati wa uwasilishaji mada kwenye semina hiyo,anasema lengo kuzuia vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi ni kwamba Tanzania inahitaji kuwa na viongozi wazalendo wenye kuchukia rushwa katika nchi yao.
Aidha, ametaja hali ya rushwa nchini, kwamba katika matokeo ya utafiti yaliyofanywa na Shirika la Transparency International tangu mwaka 2019, amesema kwamba kati ya nchi 180 mwaka huo 2019 Tanzania ilishika nafasi ya 96 kwa rushwa sawa na asilimia 37,mwaka 2020 nafasi ya 94 sawa na asilimia 38, mwaka 2021 nafasi ya 87 sawa na asilimia 39, mwaka 2022 nafasi ya 94 sawa na asilimia 38 na mwaka jana 2023 ilishika nafasi ya 87 sawa na asilimia 40.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza kwenye semina ya waandishi wa habari.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza kwenye semina ya waandishi wa habari.
Naibu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja akizungumza semina hiyo.
Mkuu wa dawati elimu kwa umma kutoka Takukuru Mohamed Doo akiwasilisha mada kwenye semina hiyo.
Waandishi wa habari wakiendelea na Semina kutoka Takukuru.
Picha za pamoja zikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464