PACESH WATAKA HAKI ITENDEKE BINTI ALIYEFANYIWA UKATILI KWA KUBAKWA NA KULAWITIWA NA VIJANA WATANO WANAODAIWA NI WANAJESHI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
SHIRIKA la kutoa huduma ya msaada wa kisheria mkoani Shinyanga (PACESH)wameungana na wadau mbalimbali ambao wamelaani tukio la binti kubakwa na kulawitiwa jijini dar es salaam na vijana watano ambao wanadaiwa ni wWanajeshi na kisha kumrekodi video na kuisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii,huku wakiomba haki itendeke juu ya tukio hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la PACESHI John Shija, ametoa tamko la kulaani tukio hilo leo Agosti 9,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kwa kauli moja wanaungana na wadau wote ambao wamelaani tukio hilo la kinyama alilofanyiwa binti huyo (jina limehifadhiwa),huku akiomba vyombo vyote vinavyopaswa kushughulikia jambo hilo vihakikishe vinatimiza wajibu wake kikamilifu na asiwepo mtu wa kukalia, kuchezea na kufumbia macho bali haki itendeke.
“Kwa masikitiko Makubwa sisi watoa huduma na wasaidizi wa kisheria Mkoa wa Shinyanga tumeumizwa sana kwa kitendo kilichosababishwa kusambaa kwa video ya binti ambaye amefanyiwa ukatili mkubwa ikijumuisha Ubakaji na ulawiti uliofanywa na vijana wanaosadikiwa kuwa watano kwa maelekezo maalumu kutoka kwa mmoja wa wanawake kama sehemu ya adhabu kwa kuwa anatembea na mume wake”amesema Shija.
“Kitendo hicho si chakulaani tu bali ni cha kukemea vikali na kuchukulia hatua kali za kisheria, kwakuwa kitendo hicho kimekwenda kinyume cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya 1977, ibara ya 5 (c) na (e) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2022 kwa kuwa matendo yote hayo yamejinaishwa na sheria hiyo, sambamba na hilo sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyorekebishwa 2022 katika kif cha 31 kinatoa adhabu kwa watenda makosa ya ubakaji wa kundi,”ameongeza.
Aidha, amesema vitendo hivyo pia vinafedhehesha nchi kwa kuwa imejinasibu kulinda haki za binadamu dhidi ya ukatili, udhalilishaji, na inanyong’onyesha jitihada za nchi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ameanzisha mikakati mbalimbali ya kushughulikia ukatili wa kijinsia ikiwemo kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya mama Samia Legal Aid Campain.
Aidha, tukio la binti huyo kufanyiwa ukatili lilitokea Agost 3mwaka huu Jijiji Dar es salaam wilaya ya Temeke Mtaa wa Yombo.