Header Ads Widget

RUTAZIKA AFUNGUA MAFUNZO YA AWALI YA UALIMU NA UAMUZI WA MPIRA WA MIKONO

Rutazika Afungua Mafunzo ya Awali ya Ualimu na Uamuzi wa Mpira wa Mikono

Na Paul Kasembo, SHY RS.

Afisa Elimu Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Dedan Rutazika, aliye mwakilishi wa Dafroza Ndalichako, Katibu Tawala Msaidizi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mkoa wa Shinyanga, amefungua rasmi mafunzo ya awali ya ualimu na uamuzi wa mpira wa mikono.

Mafunzo haya yanaendelea katika Shule ya Sekondari Uhuru na yanawahusisha walimu kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani Shinyanga, pamoja na wale kutoka Mkoa wa Simiyu na shule binafsi, ikiwemo Kom Sekondari. Mkufunzi wa mafunzo haya ni Emmanuel Majura kutoka Chama cha Mpira wa Mikono Taifa (TAHA).

Akizungumza katika hafla hiyo, Rutazika amewahimiza walimu kutumia maarifa watakayopata katika mafunzo haya kwa ufanisi ili kuhakikisha yanaongeza tija katika shule wanazotoka. Aliweka wazi matarajio yake kuwa elimu hii itachangia katika kufanya vizuri kwa wanafunzi katika mashindano yajayo mwaka 2025.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mikono Mkoa wa Shinyanga, Mtaki Musiba, alithibitisha kupokea maoni na ushauri ulioelekezwa, akiahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kukuza michezo ya mpira wa mikono mkoani Shinyanga.

Bi. Jesca Simuchile, Afisa Michezo Mkoa wa Shinyanga, amesema kuwa mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Prof. Siza Tumbo, kuhusu kuanzisha programu maalum ya kuibua, kukuza, na kuimarisha michezo mashuleni. Michezo inatambuliwa kama chanzo cha afya, ajira, na amani.

Post a Comment

0 Comments