SHYDC WATIA FORA MIRADI MWENGE WA UHURU
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MWENGE wa uhuru umekimbizwa kilomita 160 katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, na kumulika miradi 14 ya maendeleo, na miradi yote imepita kwa kishindo hakuna hata mmoja uliokataliwa.
Mbizo hizo za Mwenge wa uhuru wilaya ya Shinyanga zimekimbizwa leo Agosti 12,2024 na wakimbiza mwenge wa uhuru kitaifa Sita wakiongozwa na kiongozi wao Godfrey Mnzava.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Kalekwa Kasanga, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mwenge huo na Mkurugenzi wa halmashauri manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, amesema utakimbizwa kilomita 160 na kupitia miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 1.7.
“Miradi hii 14 ambayo itapitiwa na mwenge wa uhuru, miwili itawekewa jiwe la msingi, miwili mingine kufunguliwa, mitatu itazinduliwa na miradi 7 kukaguliwa,”amesema Dk.Kasanga.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Godfrey Mnzava, akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye miradi hiyo, ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa kuwa na miradi mizuri.
Amesema miradi yote ambayo imepitiwa na mwenge wa uhuru inapaswa kutunzwa, kulindwa na kuendelezwa ili ipate kutoa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumzia wakati akiweka jiwe la msingi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Shilabela, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutenga fedha za mapato yake ya ndani na kujenga vyumba hivyo na kuawekea mazingira mazuri wanafunzi ya kusoma na kutimiza ndoto zao.
“Katika shule hii ya Shulabela naona tena kuna vyumba vingine viwili ambayo vilinzishwa kwa nguvu za wananchi naomba na vinyewe mvimalizie kuvijenga,na pia nimefurahishwa kwamba mmetenga tena Sh.milioni 26 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati,”amesema Mnzava.
Katika hatua nyingine akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalumu shule ya msingi Iselamagazi, amewataka wazazi kuwapeleka shule watoto wenye uhitaji ili wasome kama watoto wengine na kutimiza ndoto zao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akizungumzia suala la watoto wenye uhitaji,amesema wazazi wanapaswa kubadilika na kutowaficha watoto hao ndani, bali wanapaswa kuwapeleka shuleni hapo ambapo watasoma na kuishi hapo hapo.
Aidha,miradi iliyomulikwa na mwenge wa uhuru katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ni ya elimu, ikiwamo ufunguzi wa klabu za rushwa na mazingira,miradi ya vijana,afya,maji, na miundombinu ya barabara.
Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru 2024 inasema"Tunza mazingira na Shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu"
Mwenge huo wa uhuru kesho utakimbizwa katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.