Header Ads Widget

SHYDC WAPONGEZWA KUVUKA LENGO LA UKUSANYAJI MAPATO YA NDANI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2023/2024 KWA ASILIMIA 101

SHYDC wavuka lengo ukusanyaji mapato ya ndani asilimia 101

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mkurugezi wa Shydc Dk. Kalekwa Kasanga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Shinyanga wamepongezwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji mapato ya ndani kwa asilimia 101 katika mwaka wa fedha 2023/2024 unaoishia juni 30.

Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 21,2024 kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje,akizungumza wakati wa kufunga kikao cha baraza la madiwani,amesema anampongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na menejimenti nzima kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 na kuvuka lengo kwa asilimia 101.

“Mapato ndiyo muhimili wa halmashauri pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ukamilishaji wa maboma,”amesema Mboje.
“Katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 ongezeni kasi na kukusanya mapato mengi zaidi na kuendelea kuvuka lengo, na zile fedha asilimia 40 ambazo zinatokana na ukusanyaji wa mapato mzielekeze kwenye shughuli za maendeleo kama ilivyo kwa mujibu wa sheria,”ameongeza.

Aidha,amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuendelea kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato, huku akiwasihi pia madiwani waendelee kushirikiana na Mkurugenzi katika ukusanyaji huo wa mapato, na kwamba pale wanapo ona kuna viashiria ya upotevu wowote wasisite kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga naye alisisitiza kuwapo na ushirikiano kama timu ya pamoja kati ya madiwani na watendaji wa halmashauri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, na kwamba bila ya mapato halmashauri haiwezi kufikia malengo.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga, amesema halmashauri hiyo wataendelea na kasi hiyo ya ukusanyaji mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha, na kwamba katika hilo tayari watumishi wanne ambao walikuwa wakituhumiwa kuwa na mashine feki ya ukusanyaji mapato (Pos) wapo kwenye mikono ya sheria.
Aidha,amesema licha ya wao kuwa na juhudi kubwa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, pia wanampongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi wilayani Shinyanga na kutekelezwa miradi mingi ya maendeleo.

Katika kikao hicho cha baraza la madiwani viongozi mbalimbali wakitoa salamu, wametua fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kwamba wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambalo limeanza leo Agosti 21 hadi tarehe 27,2024.
Baraza hilo la madiwani pia ziliwasilishwa taarifa mbalimbali ikiwamo ya Kamati ya fedha, uchumi, ujenzi na mazingira, ukimwi pamoja na kamati ya maadili.

Halmashuri ya wilaya ya Shinyanga katika mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi kilichopangwa kukusanywa ni Sh.bilioni 3.255, lakini hadi kufikia juni 30,2024 walikusanya Sh.bilioni 3.288 sawa na asilimia 101.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Kalekwa Kasanga akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga Chrtistina Mzava akitoa salamu za viongozi kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akitoa salamu za viongozi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Shinyanga likiendelea.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha baraza.

Post a Comment

0 Comments