NICODEMUS SIMON ASHINDA KWA KISHINDO NAFASI YA UMAKAMU MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA
BARAZA la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, limefanya uchaguzi wa kumchagua makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Uchaguzi huo umefanyika leo Agosti 22,2024 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo Aaron Laizer akimwakilisha Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga, amesema jina la Mgombea lililorudi ni moja kutoka Chama cha Mapinduzi kuwa ni Nicodemus Simon, ambaye atapigiwa kura za ndiyo au hapana.
Akitangaza matokeo hayo ya uchaguzi, amesema idadi ya wapiga kura walikuwa 35, na kura za ndiyo zilizopigwa ni 35 na hakuna kura ya hapana.
“kwa mamlaka ambayo nimepewa kama msimamizi wa uchaguzi huu, namtangaza ramsi Nicodemas Simon kuwa ameshinda nafasi ya Umakamu Mwenyekiti kwa asilimia 100,”amesema Laizer.
Katika uchaguzi huo ziliundwa pia kamati mbalimbali za madiwani ikiwamo kamati ya fedha,uongozi na mipango, kamati nyingine ni afya,elimu na maji,nyingine uchumi,uongozi na mazingira.
Kamati zingine ni kamati shirikishi ya kudhibiti ukimwi pamoja na kamati ya maadili ya madiwani.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Nicodemus Simon ambaye pia ni Diwani wa Masengwa, akizungumza mara baada ya kutangazwa kushinda nafasi hiyo kwa awamu nyingine, ambayo atadumu kwa muda wa mwaka mmoja tena, amewashukuru madiwani pamoja na Chama kwa kumuamini katika kuitumikia halmashauri.
Ameahidi kwamba ataendelea kufanya kazi kwa ushirikiamo mzuri na Mwenyekiti, Mkurugenzi wa halmashauri, Watumishi, pamoja na kuwaunganisha madiwani kuwa wamoja, na kusimamia kasi ya ukusanyaji mapato.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Ernestina Richard, amepongeza uchaguzi huo kufanyika kwa amani, huku akiwasisitiza Madiwani kwenda kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza kwenye baraza la madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa halamshauri ya wilaya ya Shinyanga Mathew Kayanda akizungumza kwenye baraza hilo.
Msimamizi wa uchaguzi Aaron Laizer akitangaza matokeo.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nicodemus Simon akizungumza mara baada ya kutangazwa kushinda nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa halmashauri kwa awamu nyingine tena.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye uchaguzi wa kumchagua Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kumpigia kura za ndiyo au hapana.
upigaji wa kura ukiendelea.