Header Ads Widget

VIONGOZI AZAKI WASHIRIKI KIKAO CHA BUNGE WAKATI WA UPITISHWAJI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA ZINAZOHUSU ULINZI WA MTOTO

VIONGOZI AZAKI WASHIRIKI KIKAO CHA BUNGE WAKATI WA UPITISHWAJI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA ZINAZOHUSU ULINZI WA MTOTO

Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI mbalimbali kutoka Asasi za kiraia wameshiriki kikao cha Bunge Jijini Dodoma kwa kufuatilia uwasilishwaji na upitishwaji wa muswada wa marekebisho ya sheria zinazohusu ulinzi wa mtoto, akiwamo Mkurugenzi wa Shirika la TYC la Shinyanga Lucas Daudi.
Wameshiriki kikao hicho cha bunge jana Agosti 30,2024 Jijini Dodoma,huku wakipongeza muswada huo kwamba utamlinda mtoto hususani dhidi ya vitendo vya ukatili.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima akiwasilisha maelezo ya muswada huo jana bungeni, amesema Kifungu cha 13 cha sheria ya makosa ya kimtandao kimeandikwa upya na kuweka masharti yanayohusiana na makosa ya unyanyasaji na utumikishaji wa kingono kwa watoto kwa kutumia nyenzo za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
“Lengo ni kuwalinda watoto kutokana na kuwepo kwa ongezeko la matukio ya uhalifu wa kingono dhidi ya watoto kupitia nyenzo za TEHAMA zinazotumika kuwashawishi, kuwatishia au kuwaonesha watoto ponografia kwa lengo la kuwashawishi kushiriki katika matendo ya kingono,”amesema Dk.Gwajima

Amesema yamewekwa masharti yanayozuia mtu au mfumo wa kompyuta kutekeleza kitendo cha kigaidi na kuweka adhabu kwa mtu anayekiuka masharti hayo ili kudhibiti na kuzuia vitendo hivyo vinavyoweza kutendeka kwa njia ya kompyuta au mifumo ya kompyuta.
“Kifungu cha 49 kimeandikwa upya ili kuweka masharti yanayohusu adhabu kwenye makosa yanayotendwa na kampuni au taasisi. Lengo la marekebisho haya ni kuainisha namna ya kushughulikia uhalifu unaotendwa na kampuni au taasisi na kuhakikisha kuwa wakurugenzi wa kampuni wanawajibika kwa uhalifu wa kimtandao unaofanywa na kampuni au taasisi wanazozisimamia,”amesema.

Aidha, amesema muswada umerekebisha mamlaka ya kufifilisha makosa yasihusishe makosa ya udhalilishaji wa kingono kwa watoto ili kufanya adhabu kwa makosa ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto itolewe na mahakama pekee kutokana na uzito wa makosa hayo.
“Pia tunapendekeza kuondoa dhana ya Shule za Maadilisho na badala yake kuweka dhana iliyokusudiwa ambayo ni Makao ya Malezi ya Watoto waliotoroka kutoka sehemu waliyowekwa kwa amri ya mahakama ya uangalizi baada ya kuondolewa kwenye familia zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uhanga wa ukatili, mazingira hatarishi,” amesema Dk.Gwajima.

Kadhalika, amesema muswada umeongeza sharti la ulazima kwa mahakama kuzingatia taarifa ya uchunguzi wa kitaalamu kutoka kwa afisa ustawi wa jamii wakati wa kutoa amri ya kugharamia vipimo vya vinasaba ili kuiwezesha mahakama kufikia uamuzi wa haki na unaotekelezeka.
“Kifungu cha 45 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuweka masharti yanayomtaka afisa ustawi wa jamii kuandaa taarifa ya uchunguzi kwa ajili ya kutumika mahakamani wakati wa mashauri yanayohusu malezi, matunzo, uangalizi na haki ya kumuona mtoto,” amesema Dk.Gwajima.

Amebainisha kuwa lengo ni kuisaidia mahakama kupata taarifa ambazo zitaiwezesha kutoa uamuzi wa haki na unaozingatia maslahi bora ya mtoto.
Amesema muswada unapendekeza kubainisha mamlaka za mahakama katika kushughulikia mashauri ya kuasili watoto. Aidha, mahakama ya watoto inaongezwa miongoni mwa mahakama zitakazoshughulikia mashauri hayo ili kuongeza ufanisi na kupunguza mlundikano wa mashauri katika mahakama nyingine.

“Pia inapendekezwa kuiondolea mahakama mamlaka ya kuruhusu mtoto kusafirishwa nje ya nchi wakati wa utoaji wa amri ya mpito kabla ya kukamilika kwa mchakato wa kuasili mtoto ili kuhakikisha ulinzi kwa mtoto anayekusudiwa kuasiliwa kabla ya mahakama kutoa amri ya kuasili,”amesema.
Muswada huo umeondoa mapendekezo ya kupunguza muda unaotakiwa kwa mwombaji wa kuasili mtoto asiye mtanzania kukaa nchini kutoka miaka mitatu hadi miaka miwili mfululizo.

Pia umerahisisha utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya malezi ya kambo kwa kuondoa mlolongo mrefu uliopo sasa.

Hata hivyo, Kifungu kipya cha 71A kimeongezwa kwa lengo la kuipa mahakama mamlaka ya kufuta amri ya kuasili kwa manufaa ya mtoto baada ya kupokea maombi kutoka kwa mzazi, mlezi au ndugu wa mtoto aliyeasiliwa au mtu mwingine yeyote mwenye maslahi.

“Marekebisho mengine ni kuongeza muda wa kumlea mtoto kabla ya kumuasili kutoka miezi mitatu hadi miezi sita ili kuwezesha na kurahisisha taratibu za kuasili na kulinda maslahi bora ya mtoto,”amesema.

MABARAZA YA WATOTO

Aidha, amesema Muswada huo unalenga kuanzisha na kurasimisha mabaraza ya watoto katika ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na ngazi ya Taifa ili kuwa na majukwaa yanayowafikia watoto na kujua changamoto zinazowakabili ili kuweza kuwalinda na matukio ya unyanyasaji na uhalifu katika jamii.

KUWALINDA NA UHALIFU

Kifungu cha 102 kinapendekezwa kurekebishwa kwa lengo la kumlinda mtoto dhidi ya uhalifu kwa kutoruhusu mtoto kuchangamana na wahalifu ambao ni watu wazima hata kama ni ndugu.

“Kifungu cha 103 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuweka masharti kwa mahakama kuhusu kuahirisha kesi zinazowahusu watoto wanaotuhumiwa kutenda makosa ya mauaji,”alisema.

Alieleza kuwa lengo ni kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya watoto na kuwalinda watoto hao dhidi ya kujifunza tabia za uhalifu gerezani.

Vile vile, alisema mtoto anarekebishwa nje ya mfumo wa mahakama kwa makosa madogo ili kumsaidia kubadilika kitabia kupitia mifumo ya jamii iliyopo zikiwamo ofisi za ustawi wa jamii na vilevile kupunguza muda na gharama za uendeshaji wa kesi za watoto.

Aidha, marekebisho hayo pia yanampa Jaji Mkuu mamlaka ya kutengeneza kanuni zitakazoainisha utaratibu wa kuwadodosa watoto mahakamani, huku utaratibu sahihi wa uwasilishaji wa rufaa kutoka mahakama ya mtoto kwenda mahakama kuu na kuondoa utata ukiwekwa.

WIGO WA MAKOSA

Pia amesema imependekezwa kupanua wigo wa makosa ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto ili kuongeza ulinzi kutokana na kuongezeka kwa kasi ukatili huo unaochangiwa na kukua kwa teknolojia na utandawazi.

MAKOSA YA UKEKETAJI

Pamoja na hayo, amesema Kifungu cha 158A kimefanyiwa marekebisho ili kukifanya kuwa na nguvu dhidi ya masharti ya sheria nyingine kuhusu makosa ya ukeketaji wa watoto na kutoa fidia kwa wahanga wa makosa hayo.

Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima, akiwasilisha muswada huo jana bungeni, amesema marekebisho hayo yanalenga kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti ya sheria hizo ili kumlinda mtoto dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili.

‘‘Mheshimiwa Spika Muswada wa Sheria unaohusu ulinzi wa mtoto ambao upo mbele ya Bunge lako tukufu, una mapendekezo ya kufanya maboresho katika sheria tatu, ambazo ni Sheria ya makosa ya kimtandao sura ya 443, Sheria ya mtoto sura ya 13 na Sheria ya msaada wa kisheria sura ya 21,

“Mhe. Spika madhumuni ya Muswada huu ni kuondoa mapungufu yaliyojitokeza ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto ambapo Muswada huu umegawanyika katika sehemu kuu nne ya kwanza inahusu masharti ya utangulizi yanayojumuisha jina la Muswada na sheria mbalimbali zinazopendekezwa, sehemu ya pili inapendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya makosa ya kimtandao ikiwemo kufutwa na kuboreshwa na kuongeza misamiati mipya,”amesema Dk.Gwajima.

Ameongeza kuwa sehemu ya tatu inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya mtoto sura ya 13 na sehemu ya nne inapendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya msaada wa kisheria sura ya 21’’

Muswada huo umegusa sheria tatu ambazo ni Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura ya 443; Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.

Chanzo cha story maelezo ya muswada Nipashe

Post a Comment

0 Comments