WANANCHI 8,038 WANUFAIKA NA MRADI WA MAJISAFI NA SALAMA,MRADI WA MAJI UKIZINDULIWA NA MWENGE WA UHURU

Wananchi 8,038 wanufaika na mradi wa majisafi na salama,mradi wa maji ukizinduliwa na mwenge wa uhuru

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WANANCHI wa Kata ya Mwalukwa wilayani Shinyanga katika vijiji vya Mwalukwa,Bulambila na Kadoto wamenufaika na mradi wa majisafi na salama.

Mradi huo umezinduliwa leo Agosti 12,2024 na kiongozi wa mwenge wa uhuru kitaifa Godfrey Mnzava.

awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa maji Mkurugenzi kutoka Shirika la Life Water International Tanzania Devocatus Kamara,amesema umetekelezwa na Shirika hilo kwa kushirikiana na Ruwasa pamoja na jamii kutoka vijiji hivyo vitatu.

Amesema lengo la mradi huo wa maji ni kuwawezesha wananchi wa vijiji hivyo,shule na zahanati katika maeneo husika kupata huduma ya maji safi na salama.

"Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mradi huu umegharimu kiasi cha fedha Shilingi bilioni 1.107 katika mchanganuo wa michango kama ifuatavyo, life water tumetoa sh.milioni 994.4, Ruwasa milioni 38.180 na wananchi milioni 75.0," amesema Kamara.

"Mradi huu umeanza kutoa huduma ya maji,na jumla y
a wananchi 8,038 wa Kata ya Mwalukwa katika vijiji vya Mwalukwa,Bulambila na Kadoto, wameweza kunufaika kwa kupata majisafi na salama,"ameongeza.

Aidha,ametoa shukrani kwa ushirikiano na miongozo ambayo waliipata kutoka kwa watalaamu serikalini, hadi kuukalimilisha mradi huo julai 30 mwaka huu.

Naye kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Godfrey Mnzava, amewapongeza wadau wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wananchi ikiwamo ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Pia,amewapongeza Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) wilaya ya Shinyanga, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo wa maji.

Ametoa wito kwa wananchi,kwamba waendelee kuitunza Miundombinu hiyo ya maji pamoja na vyanzo vya maji, ili kuendelea kuwa na uhakika wa kupata maji.

Mwenge wa uhuru leo unakimbizwa wilayani Shinyanga,
umbali wa kilomita 160 na kumulika miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 1.7.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464