NGOs ZAOMBA USHIRIKIANO ZAIDI NA SERIKALI




Na Mapuli Kitina Misalaba

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) Wilayani Shinyanga yameomba ushirikiano zaidi na serikali ili kufanikisha utawala bora na maendeleo endelevu.

Hayo yamesemwa leo Agosti 21, 2024, na Naibu Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la SHDEPHA, Bi. Shekha Nassoro, katika risala ya mashirika hayo kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) lililofanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga.

Amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanachangia kwa kiasi kikubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, haki za binadamu, na mazingira, huku yakiwa mstari wa mbele katika kulinda haki za binadamu yakiwemo makundi ya wanawake na watoto.

Bi. Shekha ameongeza kuwa mashirika haya yamekuwa kiungo muhimu cha maendeleo, lakini yanakutana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa miradi yao, ikiwemo uelewa mdogo wa jamii kuhusu majukumu yao na changamoto za kisheria na kiutawala.

"Mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa kiungo muhimu katika kutoa sauti kwa makundi yaliyo pembezoni na kuwa mstari wa mbele katika kulinda haki za binadamu," alisema.

“Changamoto hizi, pamoja na ushirikiano hafifu kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali ngazi za vijiji na vitongoji, zinahitaji kushughulikiwa ili tuweze kufanikisha malengo yetu ya kuleta maendeleo na kuimarisha utawala bora,” amesema Bi. Shekha.

Baadhi ya viongozi wa mashirika mbalimbali waliotoa maoni yao katika jukwaa hilo, wameeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia, ambapo wahanga wanakosa mazingira salama ya kulinda haki zao, hasa wakati wa kesi zao.

Wameiomba serikali kuweka mazingira bora zaidi ya ulinzi, ikiwemo kuanzisha nyumba salama kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

"Wahanga wa vitendo hivi wanakosa mazingira salama ya kuwalinda, ikiwemo nyumba salama wakati wa kesi zao,".

Pia walitoa ombi kwa serikali kuweka mfumo maalum wa kusaidia mashirika madogo yanayochipukia ili yaweze kushirikiana na mashirika makubwa yanapotekeleza miradi yao.

“Kuna mashirika madogo yanayojitahidi kutoa huduma katika jamii, lakini yanakabiliwa na changamoto za kifedha, tunashauri kuwe na mfumo maalum wa ushirikiano kati ya mashirika makubwa na madogo ili kuhakikisha kuna mwendelezo wa miradi hata pale mashirika makubwa yanapoondoka,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Vilevile, viongozi hao walilalamikia ucheleweshaji wa takwimu muhimu zinazohusiana na matukio ya ukatili wa kijinsia. Walipendekeza kuboreshwa kwa mfumo wa upatikanaji wa takwimu hizo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

"Tunaomba mfumo wa upatikanaji wa takwimu hizi uboreshwe ili mashirika yawe na uwezo wa kupata takwimu hizi moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa MTAKUWWA,".

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ameyapongeza mashirika hayo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuahidi ushirikiano wa karibu kati ya serikali na NGOs ili kuimarisha utawala bora na maendeleo katika Wilaya ya Shinyanga.

Amesema serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazokwamisha mashirika hayo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku akitoa wito kwa watumishi wa ngazi za chini kushirikiana na mashirika hayo kwa maslahi ya wananchi.

Kwa upande wake, Kiongozi wa NACONGO Wilaya ya Shinyanga, Bwana Lucas Daud, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano wake na kuahidi kuwa mashirika hayo yataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kufuata sheria na taratibu za nchi.

Kaulimbiu ya jukwaa hilo inasema "MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI NI WADAU MUHIMU, WASHIRIKISHWE KUIMARISHA UTAWALA BORA."

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza kwenye jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali Wilaya ya Shinyanga Agosti 21,2024.


Naibu Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la SHDEPHA, Bi. Shekha Nassoro, akisoma risala ya mashirika hayo kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) lililofanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga Agosti 21,2024.

Naibu Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la SHDEPHA, Bi. Shekha Nassoro, akisoma risala ya mashirika hayo kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) lililofanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga Agosti 21,2024.

Kiongozi wa NACONGO Wilaya ya Shinyanga, Bwana Lucas Daud, akizungumza kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) ambalolimefanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga Agosti 21,2024.

Kiongozi wa NACONGO Wilaya ya Shinyanga, Bwana Lucas Daud, akizungumza kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) ambalolimefanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga Agosti 21,2024.

Kiongozi wa NACONGO Wilaya ya Shinyanga, Bwana Lucas Daud, akizungumza kwenye Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) ambalolimefanyika katika ukumbi wa Rafiki SDO Mjini Shinyanga Agosti 21,2024.Meneja mradi wa shirika la Rafiki SDO Bi. Maria Maduhu akizungumza kwenye jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali Wilaya ya Shinyanga Agosti 21,2024.Meneja mradi wa shirika la Rafiki SDO Bi. Maria Maduhu akizungumza kwenye jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali Wilaya ya Shinyanga Agosti 21,2024.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464