HALMASHAURI YA MJI WA BABATI, YATAMBA KUANDISHA WANAFUNZI KWA ASILIMIA 103
Afisa elimu msingi wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara Simon Mumbee akizingumza na Shinyanga Press club blog
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Osterbey iliyopo Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara wakiwa uwanja wa Tanzanite Kwaraa wakifatilia matukio mbalimbali uwanjani hapo.PICHA: JALIWASON JASSONNa Jaliwason Jasson, MANYARA
HALMASHAURI ya Mji wa Babati mkoani Manyara imetamba kuandikisha wanafunzi 3,327 wa darasa la kwanza mwaka huu sawa na asilimia 103.
Akizungumza na Shinyanga Press club Blog Afisa elimu msingi wa Halmashauri hiyo Simon Mumbee amesema hayo leo katika mahojiano maalumu juu ya namna walivyofanikisha uandikishaji.
Mumbee amesema kati ya wanafunzi 3,327 wavulana walikuwa 1,686 na wasichana walikuwa 1,643 huku wao walilenga kuandikisha wanafunzi 3,262 wavulana 1,630 na wasichana 1,632 ambapo idadi hiyo ilikamilika Machi 31 mwaka huu.
Afisa elimu huyo amesema vitu vilivyoisaidia Halmashauri kufikia lengo ni kuanza mapema mwezi Septemba uandikishaji, kushirikiana na viongozi wa mitaa, kata na walimu pamoja na wazazi.
Aidha amesema idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa wote wanasoma hadi darasa la saba na huwa inaongezeka kutokana na wengine kuhamia.
Naye Mshauri wa malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM)kutoka Shirika la Children Incrossfire ( CIC) Davis Gisuka akizungumzia mafanikio hayo amesema inaonekana wazazi wana uelewa mpana juu ya elimu ndio maana wameandikisha kwa wingi watoto wao.
Mkazi wa Kijiji cha Nakwa Zena Said amesema wazazi kuandikisha kwa wingi wanafunzi wa darasa la kwanza ni kutokana na watu kujua umuhimu wa elimu.
Said amesema wapo wazazi wengine ambao uitumia shule kama walezi wa watoto wao.
Mkazi wa Mtaa wa Komoto Patrick Urasa amesema Halmashauri hii kufanikiwa kuandikisha kwa wingi wanafunzi wa darasa la kwanza ni kwa kuwa ipo Mjini.
Kwa mujibu wa sera ya elimu ya mwaka 2014 inaeleza kuwa serikali itaweka utaratibu wa elimu msingi kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kutolewa kwa miaka 10 na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na maendeleo na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.
Pia kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu(SDG) haki ya watoto wote ya kupata elimu siyo tu lengo la nne la ajenda ya 2030 bali imewekwa katika Mkataba wa haki za mtoto na mikataba na matamko mengine ya kimataifa ambayo yanahitaji elimu ya msingi iwe bure na lazima kwa wote.
Aidha inakadriwa kuwa kati ya asilimia 75 mpaka 80 ya viashiria muhimu kwa watoto katika kila Nchi hakuna takwimu za kutosha za kuonyesha maendeleo ya kutosha kwa SDG namba nne ambayo ni elimu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464