Taasisi ya Manala Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Red Cross Tanzania na Ofisi ya Mganga Mkuu Manispaa ya Kahama kupitia kitengo cha damu salama wamefanikisha zoezi la kuchangia damu kwa hiari.
Zoezi la uchangiaji damu limefanyika kata ya Kagongwa, Manispaa ya Kahama Agosti 15, 2024 wakati wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru, ambapo Mratibu wa Damu Salama Elibahati Molle amepongeza juhudi za Manala Foundation kwa kuhamasisha jamii hiyo katika kuchangia damu kwa hiari na wamekusanya unit 51 za damu.
Mkurugenzi wa Manala Foundation, Mhandisi Manala Tabu Mbumba, amesema taasisi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika nyanja mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo na ustawi wa jamii, pia kuunga juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Manala amewashukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, pamoja na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama kwa ushirikiano wao kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, Pia amewashauri wadau mbalimbali kujitokeza na kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zinazoikumba jamii.
Miongoni mwa wananchi waliochangia damu, Juma Mabula, ameeleza kuwa kupitia uhamasishaji wa taasisi ya Manala ameweza kuchangia damu ambayo inaenda kuwasaidia wahitaji.
Taasisi ya Manala Foundation imesajiliwa kitaifa na makao makuu yake yako Dar es Salaam.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464