MHE. SANGU AANIKA SULUHISHO MAKAZI YA WATUMISHI

 

Na Mwandishi wetu
“Fanyeni kazi kwa viwango vya juu hususani katika ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma na majengo ya Serikali kwa kuzingatia viwango vinavyostahiri ili tuweze kuaminiwa na kupata fedha za kuwekeza zaidi”.

Maneno hayo yalisemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu kwa menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) tarehe 19 Agosti, 2024 jijini Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kujifunza namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

Mhe. Sangu alisema WHI inaamika katika kazi na sasa inapata zabuni za kujega majengo na kusimamia kazi mbalimbali za ujenzi ikiwa kama mshauri mwelekezi, hivyo wanastahiri pongezi.

Aidha, Mhe. Sangu ametumia kikao hicho kutoa maelekezo kwa menejimenti ya WHI kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya fedha kutoka kwa watumishi wa umma waliokopeshwa nyumba ili fedha hizo ziweze kutumika katika ujenzi wa nyumba nyingine  za watumishi.

Ameongeza kwa kuwataka WHI kutengeneza utaratibu na kuingia Mikataba na Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kupata maeneo na kujenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi wa umma.

Hali kadhalika, Mkurugenzi Mtendaji wa WHI Dkt. Fred Msemwa amesema katika utekelezaji wa mpango wa makazi kwa watumishi wa umma zipo nyumba zinazojengwa na kuuzwa na nyingine haziuzwi kwa kuwa Serikali inakuwa imetoa fedha kwa ajili ya miradi maalum kwenye maeneo maalum na nyumba hizo hukabidhiwa kwa walengwa.

Vile vile, amemshukuru Mhe. Sangu kwa kufanya ziara katika taasisi hiyo na ameahidi yeye na menejimenti yake kutoa ushirikiano wa dhati wakati wote kwa manufaa ya umma.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464