Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, akiwa na viongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru wakikagua miradi mbalimbali ya manispaa ya Shinyanga
Suzy Butondo,Shinyanga press blog
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema kuwa Mwenge wa Uhuru umekimbia katika mikoa zaidi ya 22 na kukagua miradi 1,074 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.7.
Hayo ameyasema 11,8,2024 wakati akisoma taarifa yake baada ya kupokea mwenge wa uhuru katika manispaa ya Shinyanga, ambapo amesemaMwenge huo umekimbia katikamikoa zaidi ya 22 na kukagua miradi 1,074 yenye thamani ya shilingi trioni 10.7.
Amesema katika miradi hiyo, miradi 13 yenye thamani ya shilingi bilioni 7.6 imekutwa na dosari mbalimbali na kwamba Mwenge wa Uhuru umepita kwenye Halmashauri 131 na bado unatarajiwa kufika katika Halmashauri 64 kati ya 195 zilizopangwa.
Katambi amesema kuwa miradi iliyo na dosari tayari imechukuliwa hatua stahiki na mamlaka husika zimepewa maagizo ya kuirekebisha mara moja.
Miongoni mwa miradi iliyokutwa na dosari ni mradi wa maji katika Manispaa ya Morogoro, pamoja na miradi mingine iliyopo mikoa ya Njombe, Dodoma, Singida, Mara, na Itilima mkoani Simiyu.
Aidha Katambi ameongeza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kiutawala dhidi ya watumishi wa umma watakaobainika kuhusika na kasoro hizo.
" Kwa kweli hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria na kiutawala pale ambapo mradi utakutwa na dosari na watumishi wa umma wamehusika katika mradi huo ," amesema Katambi,
"Fedha zilizotolewa na serikali zinapaswa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi bila kuleta hasara yoyote ile,"ameongeza Naibu waziri Katambi.
Hata hivyo katika Manispaa ya Shinyanga, mwenge wa uhuru umemulika miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 4.2. na unaendelea na kazi zake katika mikoa na Halmashauri zilizobaki, ukilenga kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa inakaguliwa na kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.