Mutayoba Arbogast, Bukoba
HATIMAYE kilio cha muda mrefu kutoka kwa watu wenye ualbino, kuwa wanaishi mashakani kwa hofu ya kuuawa na kufanyiwa ukatili mwingine, wakidai serikali haikuwa na mpango madhubuti na wa muda mrefu wa kuwalinda, sasa kilio hicho kimepatiwa ufumbuzi, baada ya kuzinduliwa kampeni maalum yenye mikakati madhubuti, kuwalinda watu wenye ualbino.
Kampeni hiyo imezinduliwa wilayani Muleba, mkoani Kagera tarehe 9 Julai mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratias Ndejembi, ambaye sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi.
Kampeni hiyo imekuja siku hadhaa baada ya kuibuka upya hofu kwenye jamii, iliyotokana na kuuawa mtoto wa kike mwenye ualbino, Asimwe Novart (2.5), mkazi wa Kamachumu wilayani Muleba.
Asimwe alichukuliwa kwa nguvu kutoka katika makazi yao na washambuliaji wasiojulikana katika utekaji nyara huo wa kutisha ulitokea usiku Mei 30, 2024, na hatimaye kukutwa katani humo humo akiwa ameuawa na mwili wake ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo vyake baada ya siku 19 za kuchukuliwa kwake na maharamia hao.
Sakata hilo la kuhuzunisha kuhusu kuuawa kwa Asimwe ni ukumbusho wa changamoto zinazoendelea kuwakabili watu wenye ualbino nchini Tanzania. Licha ya juhudi za pamoja za serikali za kukomesha ukatili dhidi ya watu hao walio katika mazingira magumu, wimbi la hivi karibuni la unajisi mkubwa unaolenga mabaki ya albino limezusha hofu na kuzua hasira ndani ya jamii ya albino.
Mwandishi wa makala hii alifanikiwa kufanya mahojiano na viongozi wa Chama cha watu wenye ualbino, Tanzania Albinism Society (TAS), Mwenyekiti Godson Mollel, Makamu mwenyekiti Alfred Kapole, na Katibu wa chama hicho kwa mkoa wa Kagera Ignas Lugemalira, mjini Bukoba tarehe 22 Juni mwaka huu, wakati wakiwa katika harakati za kufuatilia mauaji ya mtoto Asimwe.
Viongozi hao, pamoja na mambo mengine, walisisitiza umuhimu wa serikali kuwa na mpango mkakati wa muda mrefu wa kuwalinda watu wenye ualbino badala ya kuwa na mipango ya dharura nay a muda mfupi ambayo haijazaa matunda, na hivyo unyanyapaa, ukatili na mauaji dhidi yao vimeendelea kuwakabili.
Mazungumzo yao yalihusishwa pia kwenye kipindi mubashara cha redio kilichorushwa siku hiyo na Redio Shnuz FM ya mjini Bukoba, kipindi kilichoandaliwa na wadau-watekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), kilichoangazia ULINZI NA USALAMA WA WATOTO HASA WAKATI WA MAJANGA.
Kwa mujibu wa PJT-MMMAM inaelezwa kuwa "....kutokuwepo na nyenzo za utambuzi wa mapema wa ulemavu katika vituo vya afya, vituo vya kulelea watoto wadogo mchana , elimu ya awali na elimu ya msingi inaleta changamoto kubwa kwenye kuwasaidia watoto wadogo.Watoto wenye ulemavu, ikijumuisha watoto wenye ulemavu wa viungo na wenye ualbino wamekuwa wakitengwa kupata huduma muhimu kwa ukuaji wao"
Hata hivyo serikali ilisikia kilio cha wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari juu ya usalama wa watu wenye ulemavu wa ngozi, na ikaja na mikakati maalum, ambayo, wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo maalum, waziri Ndejembi aliitaja kuwa ni kufanya operesheni ya kuwakamata waganga wa tiba asili na tiba mbadala wasio na leseni, na wale wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi ambayo imetajwa kuwa chanzo cha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Akawaagiza wakuu wote wa mikoa hapa nchini kutimiza jukumu hilo.
"Nawaagiza wakuu wa mikoa kufanya operesheni maalum ya kuwakamata waganga wa tiba asilia na tiba mbadala wanaojishughulisha na ramli chonganishi, wasio na vibali chini ya Wizara ya Afya na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,watu wenye ualbino wana haki ya kuishi kama mimi na wewe hivyo ukatili dhidi yao kwasababu ya tamaa havina nafasi "aliagiza Ndejembi
Hatua nyingine ni kuimarisha Kamati zenye watu wenye ulemavu katika halmashauri zote za wilaya, kwa mujibu wa sheria namba 19 ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu.Katika kuinua hali za kiuchumi kwa watu wenye ualbino, Serikali itatoa ruzuku kwa chama chao yaani Tanzania Albino Societ (TAS), ili kuinua kipato chao.
Aidha, serikali inaanzisha mpango wa kuanza usajili wa watu wenye ualbino kwa njia ya kielektroniki ili kurahisisha kutambuliwa idadi yao ili kuweza kuwahudumia kwa urahisi.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TAS Alfred Kapole aliiomba jamii kuwalinda watu wenye ualibino na sio kuacha jukumu hilo mikononi mwa jeshi la polisi tu.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa alisema mkoa wa Kagera ni mkoa wa kwanza kutekeleza maagizoya Serikali ya kuweka mikakati madhubuti ya kulinda watu wenye ualbino, na akawahimiza watendaji walio mikoa mingine kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wanalindwa na kujumuishwa katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Vyombo vya ulinzi, vimefanyia kazi kwa umakini tukio la kutekwa mtoto Aswimwe. Taarifa iliyotolewa na Msemaji waJeshi la polisi, David Misime imesema watuhumiwa 9 wamekamatwa ambao ni baba mzazi wa mtoto huyo, Novart Venant, Desideri Evarist ambaye ni Mganga wa jadi, Padre Elipidius Rwegoshora na Dastan Kaiza.
Watuhumiwa wengine ni Faswiru Athuman, Gozibert Alkadi, Rwenyagira Burkadi, Ramadhani Selestine na Nurduni Hamada. Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kuua bila kukusudia, shauri namba 17440.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeitaka serikali kuweka mazingira imara kudhibiti matukio hayo ya kikatili wakinukuu takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi kwa mwaka 2003, kuwa watoto 73 walitekwa nchini.
Mjumbe wa mtandao huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi habari mkoa wa Mwanza, Edwin Soko, alisema kati ya watoto hao, 33 walitekwa kutoka Kanda ya Ziwa na kuwa kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2024, walitekwa watu 20 wenye ualbino katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku mwaka huu yakitokea matukio matatu kwa mkupuo.
Ni kupitia hatua za pamoj tunaweza kutumaini kujenga mustakabali ulio salama na wenye usawa zaidi kwa raia wote, bila kujali rangi ya ngozi au sura ya kimwili. Katika uso wa giza hilo lililoenea, wananchi lazima wasimame katika mshikamano na jumuiya ya albino, kudai haki kwa Asimwe Novath. na wale wote ambao wameangukia kwenye janga la kudhulumiwa haki yao ya msingi kabisa. Haki ya kuishi.
Picha:
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464