SHILUKA AWATAKA WAHITIMU CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KOLANDOTO KUTUMIA ELIMU YAO KWA MANUFAA YA JAMII

Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Paschal Shiluka amewataka wahitimu kutumia elimu kwa manufaa ya jamii

Na Elisha Shambiti
MKUU wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Shinyanga Mwl. Paschal Shiluka,amewataka wahitimu wa kozi za afya katika chuo hicho kutotazama elimu waliyoipata kama mali yao binafsi bali kama rasilimali ya jamii.

Akizungumza jana kwenye mahafali ya kumi na mbili (12) ya chuo hicho, Mwl. Shiluka amewashauri wahitimu kutumia elimu yao kutatua changamoto za kiafya katika jamii.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho, Dk. Luzila John, amesisitiza umuhimu wa wahitimu, kuwa mabalozi wema wa chuo chao kwa kuzingatia maadili mema, pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

Katibu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Mch. Mwl. Josephales Mtebe, ametoa wito kwa wahitimu kuonyesha upendo na ukarimu kwa wagonjwa, ili kuwawezesha kupata nafuu kabla ya kupatiwa matibabu.
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mzava, ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, amewashauri wahitimu kujitegemea wenyewe kwa kutumia fursa mbalimbali za mikopo kwa vijana zinazotolewa na serikali, kwani serikali haiwezi kuwaajiri wote mara moja.

Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, kilichoanzishwa mwaka 1957 na Kanisa la AICT na kilianza udahili wa wanafunzi kumi na mbili, katika mahafali haya wanachuo 316 wamehitimu kutoka kozi za maabara ya viwanda, uuguzi na ukunga, maabara ya binadamu, utabibu, na famasia.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mahafali yakiendelea.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464