TAPO LA SHYEVAWC WAPONGEZA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA ULINZI NA USALAMA WA MTOTO

 TAPO LA SHYEVAWC WAPONGEZA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA ULINZI NA USALAMA WA MTOTO

         

Wajumbe wa Tapo la SHYEVAWC wakifatilia kikao cha bunge Muswada wa marekebisho ya sheria ya ulinzi na usalama wa Mtoto ya  Mwaka 2024 

   Na; Mwandishi wetu,

Kikundi kazi cha asasi za kirai zinazohusika na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (SHYEVAWC) kimepongeza bunge kwa kupitisha Muswada wa marekebisho ya sheria ya ulinzi na usalama wa Mtoto ya  Mwaka 2024 ili kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini na kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto.

Hayo yameajili leo agosti 30 wakati wajumbe wa kikundi kazi hicho walipokutana mkoani Shinyanga kufuatilia Bunge la 12 kikao cha nne Mkutano wa 16 kwa njia ya Televisheni (TV) katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Rafiki SDO Kitangili,manispaa ya Shinyanga.

 Wadau hao wameipongeza serikali kwa kupitisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya ulinzi na usalama wa Mtoto unaojumuisha maoni mbalimbali waliyoyatoa ili kuendelea kuimarisha ulinzi wa mtoto.

Mwenyekiti wa (SHY EVAWC),Jonathan Manyama Kifunda ameiomba  serikali iendelee kuweka mazingira rafiki zaidi kwa taasisi zinazoshughulikia maswala ya ulinzi kwa watoto ili kurahisisha utendaji wa kazi.

Mwenyekiti wa (SHY EVAWC),Jonathan Manyama Kifunda akiongoza kikao kupokea maoni ya wajumbe.

sisi kama umoja wa mashirika tumepokea kwa furaha sana kwa sababu ni kitu ambacho tulikuwa tunakitarajia na katika uzoefu tulionao wa utekelezaji wa miradi kama hii tumekuwa tunapambana na kukutana na changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zinakosa msingi wa kisheria unaowafanya watoto wasiweze kuishi kwa amani katika jamii zao"Amesema Jonathan 

"Sasa ujio wa muswada ambao kwa baadae utakuwa sheria utasaidia sana kurahisisha utendaji wa kazi kwetu sisi, wadau mbalimbali na hata serikali kwa ujumla kwa hiyo tunaiomba serikali iweke mazingira rafiki zaidi kwa watoto ili waweze kuzifikia ndoto zao katika maisha’’Amesema Jonathan

Marekebisho hayo yanagusa sheria tatu ambazo ni Sheria ya Sheria ya makosa ya kimtandao sura ya 443, Sheria ya mtoto sura ya 13 na  Sheria ya msaada wa kisheria sura ya 21.

Akiwasilisha maelezo ya Muswada huo leo tarehe 30.08.2024 Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Maendeleo,Jinsia,Wanawake na wenye Mahitaji Maalum Mhe. Dorothy Gwajima amesema marekebisho hayo yanalenga kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti ya sheria hizo ili kumlinda  mtoto dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili.

‘‘ Mheshimiwa Spika Muswada wa Sheria unaohusu ulinzi wa mtoto ambao upo mbele ya Bunge lako tukufu  unamapendekezo ya kufanya maboresho katika sheria tatu ambazo ni Sheria ya makosa ya kimtandao sura ya 443, Sheria ya mtoto sura ya 13 na  Sheria ya msaada wa kisheria sura ya 21. Mhe. Spika madhumuni ya Muswada huu ni kuondoa mapungufu yaliyojitokeza ili kuimarisha ulinzi na masrahi bora ya mtoto ambapo Muswada huu umegawanyika katika sehemu kuu nne ya kwanza inahusu masharti ya utangulizi yanayojumuisha jina la Muswada na sheria mbalimbali zinazopendekezwa, sehemu ya pili inapendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya makosa ya kimtandao ikiwemo kufutwa na kuboreshwa na kuongeza misamiati mipya, sehemu ya tatu inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya mtoto sura ya 13 na sehemu ya nne inapendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya msaada wa kisheria sura ya 21’’

Kwa upande wao,Wabunge walichangia hoja zao na kubainisha changamoto kadhaa zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa sheria hiyo  pamoja na upungufu wa maafisa ustawi na kutofanyiwa marekebisho kwa baadhi ya  vifungu vya sheria ya ndoa.

Peter Amani ,mmoja ya mjumbe wa TAPO hilo,alisema mwanga umeoneka katika kusaidia watoto na alishauri kuwa ni vema sheria zingine zinazohusu mtoto zilipaswa kujadiliwa kwa maeneo yaliyo na upungufu na kuachia mianya.

 




Wajumbe wa TAPO la SHYEVAWC wakifatilia kikao cha bunge leo agosti 30,2024

Wajumbe wakichangia hoja zao juu ya muswada wa marekebisho ya sheria ya ulinzi na usalama wa mtoto.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464