Header Ads Widget

TCRA-CCC NA FCS WASAINI MAKUBALIANO YA KUFANYA MRADI WA MIAKA 3 KUTOA ELIMU NA KUWALINDA WATUMIAJI HUDUMA SEKTA ZA MAWASILIANO

 

Wajumbe wa Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za mawasiliano Tanzania na watendaji wa Foundation for Civil Society, wakishuhudia utiwaji wa sahihi wa makubaliano ya mashirikiano Kati ya taasisi hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maigizo ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuziagiza taasisi za serikali kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ili kuweza fanikiwa kuifikia jamii nzima

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) wametia saini makubaliano ya miaka mitatu ya kushirikiana na Taasisi ya The Foundation for Civil Society (FCS) kuhakikisha juhudi za kulinda haki za Watumiaji wa huduma katika Sekta ya Mawasiliano nchini zinaimarika.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Agosti 6,2024 Jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC)  Mhe. Hawa Ng’umbi amesema yeye na bodi yake katika kutekeleza majukumu yao nakutekeleza wito wa Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuziasa taasisi za serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuwafikia wanachi.

Hawa amesema Baraza lake limeanza kutekeleza hilo kama sehemu ya jitihada za kuweza wafikia watanzania wengi na kuwafikia watanzania nchi nzima kutoa elimu ya haki na wajibu wa mtumiaji huduma za mawasiliano. 

"Ubia huu utasaidia kufika mbali zaidi na akaelezea lengo kubwa la bodi inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya Baraza hilo ni kuhakikisha kuna mabadiliko chanya kwenye baraza na kuboresha utendaji uliopo",amesema. 

Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la watumishi wa huduma za mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) Bi. Hawa Ng'umbi

Aidha amesisitiza ni kwa mara ya kwanza toka kuanzishwa kwa  bodi hiyo kufunguka nakutafuta mashirikiano na wadau wengine ili kuongeza nguvu  na kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi, hasa wa vijijini ili waone baraza lao likiwatumikia kwa ukaribu zaidi na sio kutegemea pesa kidogo za serikali katika kuendesha shughuli zake na ndio maana wamewatafuta The Foundation for Civil Society (FCS). 

Ameongeza kuwa yeye kama Mwenyekiti wa bodi ya baraza hilo ana imani The Foundation for Civil Society (FCS) watashirikiana vyema na watendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) kutekeleza mradi uliowekewa saini kwa manufaa ya watumiaji wote.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge, akizungumza katika hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo, alisema kuwa ushirikiano huo unatambua umuhimu wa kuwalinda watumiaji dhidi ya mbinu za kibiashara zisizo za haki katika soko.

 Amesema jitihada za kulinda haki za Watumiaji (consumer protection) kunachangia Maendeleo ya masoko na ukuaji wa Biashara.

"Biashara zinazoheshimu sera za kulinda Watumiaji na kuwapa wateja wao kipaumbele hujijengea hadhi na kuziweka katika nafasi nzuri kiushindani. Kuna umuhimu wa asasi za kiraia kushiriki katika kuimarisha mifumo ya kulinda na kutetea haki za Watumiaji wa huduma na bidhaa za Mawasiliano", amesema.

Amefafanua kuwa katika soko la sasa lenye mabadiliko ya haraka, uadilifu katika biashara unategemea kwa kiasi kikubwa kulinda haki za watumiaji dhidi ya mbinu zisizo za haki na udanganyifu katika biashara.

"Wafanyabiashara wana nafasi muhimu katika kuhakikisha uwazi na usahihi katika shughuli zao,kutoa taarifa sahihi na kwa wakati na kuepuka upotoshaji kuhusu bidhaa na huduma zao", amesema.

Amesema kupitia mradi huo watajenga uwezo wa asasi za kiraia kuboresha uwiano katika Sera na hatua zinazochukuliwa katika ngazi ya chini, hasa pale ambapo wadau na Watumiaji wa bidhaa wana uelewa mdogo kuhusu haki na majukumu yao ili kukuza uelewa wa watumiaji wa huduma na bidhaa.

"Watumiaji wana haki ya kupata suluhu ya haki kwa madai ya msingi, elimu na uwezo kuhusu bidhaa, huduma na haki zao na uhakika wa ubora wa bidhaa na huduma", amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCRA CCC,Mary Msuya amesema Baraza limeanzishwa kwa lengo la kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za Mawasiliano za TEHAMA, huduma za Utangazaji, huduma za posta, na vifurushi na vipeto.

Amesema Baraza linatekeleza majukumu yake ya kuwakilisha watumiaji wa huduma na bidhaa za Mawasiliano kwa kushauriana na wadau ambao ni Serikali, TCRA, watoa huduma na watumiaji wenyewe.

"Huduma za mahusiano nchini zinaongezeka kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia ambapo kwa mujibu wa TCRA kufikia June 2024 kuna Kadi za simu Milioni 76.6, watumiaji wa interneti milioni 39.3, akaunti za pesa mtandao milioni 55.7. Idadi hii itaendelea kuongezeka na huduma mpya zitaongezeka kutokana na kukua kwa teknolojia ya kidigitali.

"Ukuaji huu wa teknolojia ni muhimu hasa wakati nchi yetu imejikita kwenye uchumi wa kidigitali, mawasiliano yanawezesha kufikisha taarifa kwa wakati, uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo biashara, uzalishaji, elimu, afya na upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha," amesema.

Hatua hiyo ya FCS na TCRA-CCC inalenga kuhakikisha kunakuwepo haki na uwajibikaji katika kutoa huduma kwa watumiaji na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanaponunua na kutumia bidhaa za huduma hiyo.

     

Post a Comment

0 Comments