Baadhi ya wazazi wapewa elimu juu ya unyonyeshaji watoto Halmashauri Ushetu
Na Kareny Masasy,
HAPA nchini Tanzania tangu mwaka 2016 wiki ya unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani imekuwa ikiendana na Malengo ya Maendeleo endelevu (Sustainable Develepment Goals) yanayojumuisha kiashiria cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee nakuhakikisha suala la unyonyweshaji linapewa kipaumbele.
Ukosefu wa elimu sahihi ya unyonyeshaji kwa baadhi ya wazazi Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga umesababisha kuanza kuwalisha watoto vyakula vya mbadala wa maziwa kabla ya umri wa miezi sita kutimia.
Mkazi wa kijiji cha Iyogo Amina Mussa anasema miaka ya nyuma walikuwa wakinyonyesha mtoto mpaka anafikia umri wa miaka mitatu lakini wazazi wa wasasa wanadai majukumu yamewaelemea.
“Wazazi wa sasa wanalazimika kuachisha kwa visingizio vingi kwa kueleza matatizo ili hali asimyonyeshe mtoto na anapo kaa muda mrefu shambani maziwa anayakamua chini huo nao ni ukatili kwa mtoto”anasema Musa.
Zubeda Julias anasema wazazi wengine wanakoroga uji mwepesi uliochujwa na kunywesha mtoto kwa madai hashibi anaponyonya maziwa ya mama pekee.
Charles Magili anasema wazazi walio bahatika kuwa na mifugo au fedha wamekuwa wakitumia njia ya kuwapa maziwa ya ng’ombe nakuwaacha watoto nyumbani kuwa maziwa hayo watakunywa na kushiba.
Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Ushetu Hadija Nasibu anawashauri wazazi siku ya unyonyeshaji iliyofanyika kwenye kijiji cha Uyongo nakueleza upo umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee mpaka afikishe umri wa miezi sita.
Nasibu anasema siku moja alibainika mtoto mwenye mwezi mmoja aliletwa hospitalini aliyekuwa akipewa uji matokeo yake tumbo likajaa na mtoto kulia muda wote wanapo waambia wataalamu usimpe kitu chochote basi wafuate maelekezo.
“Wastani wa watoto wanne hadi watano kati ya kumi wananyinyeshwa kwa kipindi cha miezi sita pekee ya mwanzo huku sehemu kubwa ya watoto hupewa maji wakiwa na miezi miwili na wengine kuanzishiwa maziwa na kuwachwa kunyonyeshwa tena”anasema Nasibu.
Nasibu anasema hali hiyo inasababisha kuwepo ongezeko la watoto wenye lishe duni hivyo watakuwa wanatoa elimu ya unyonyeshaji na makundi ya vyakula vya aina mbalimbali wakati wa mahudhurio ya kliniki.
“Watafundishwa namna ya kuandaa vyakula kwa mama wanaonyonyesha na wajawazito pindi watakapo fanya mahudhurio yote ya kliniki”anasema Nasibu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu Dk Jenviva Gabriel anasema wazazi wengi wamekuwa wakiacha kunyonyesha watoto na kukimbilia shambani kulima au kuvuna wakati huo mtoto anahitaji kunyonyeshwa kwani maziwa ya mama yanamfanya mtoto kukomaza ubongo wake.
“Ninawataka kuzingatia suala la unyonyeshaji kama ambavyo wamekuwa wakikumbushwa wawapo kliniki kwani mtoto asiponyonya ipasavyo anakuwa hana uwezo wa kutunza kumbukumbu na kile atakachokuwa anafundishwa awapo darasani kukiweka kwenye ubongo wake”anasema Gabriel.
Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema asilimia 72 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaupungufu wa damu ikiwa baadhi ya wazazi wamekuwa hawanyonyeshi kwa utaratibu unaotakiwa maziwa ya mama ambayo yana virutubishi vingi.
Hamis anasema mkoa wa Shinyanga una asilimia 83 ya watoto wanaonyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita pekee.
Hamis anasema watoto wenye umri wa miezi 0 hadi 23 ni asilimia 99 walioanzishiwa maziwa ya mama ndani ya saa moja na walioendelea kunyonya baada ya saa moja ni asilimia 3.9.
“Waliondelea kunyonya baada ya mwaka mmoja ni asilimia 78 wazazi wanaelezwa umuhimu wa kunyonyesha watoto baada ya kuazaliwa na baada ya kufikisha umri wa mwaka mmoja ikiwa wataalamu kwenye vituo vya afya wameendelea kutoa elimu”anasema Hamis.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dk Justina Tizeba anasema wazazi wamekuwa chanzo cha kuwapatia watoto magonjwa yasiyo ambukizwa hasa upungufu wa damu na udumavu.
“ukosefu wa madini ya vitamin A utamfanya mtoto kuwa na uoni hafifu au kutokuona kabisa na ukosefu wa madini chuma unachangia upungufu wa damu mwilini na madini joto unamfanya mtoto kutokukua vizuri hivyo lazima anyonyeshwe vizuri maziwa ya mama ”anasema DK Tizeba.
Kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe nchini( TFNC ) inaeleza mnamo mwaka 1990 mkutano wa wataalamu wa lishe ulifanyika nchini Italia lengo kujadili mwelekeo wa kisera kuhusu kuendeleza unyonyeshaji Watoto maziwa ya mama.
Mkutano huo uliohisaniwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO (Shirika la Afya Duniani) na UNICEF (Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto) Ulifanyika mwaka 1990
Azimio lililopitishwa na nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kuweza kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo .
Kwa mujibu wa shirika la Utangazaji Nchini Uingereza( BBC) limeeleza kwa takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) zinakadiria kuwa unyonyeshaji usio wa kutosha husababisha asilimia 16 ya vifo vya watoto kila mwaka.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza akina mama kuungwa mkono na jamii, familia, na wahudumu wa afya wakati wa kunyonyesha.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464