KATAMBI AWAPONGEZA MAWAKALA WA CCM KWA USIMAMIZI MZURI UANDIKISHAJI WANANCHI DAFTARI LA MPIGA KURA, ATOA ZAWADI YA SH.MILIONI 10
MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, amewashukuru mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa usimamizi mzuri wa uandikishaj wananchi kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
Katambi ametoa shukrani hizo jana Agosti 31,2024 alipokutana na mawakala hao wapatao 400 katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa chama wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa Mabala Mlolwa.
Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, amesema mchango wa mawakala hao ni mkubwa na wenye kuleta maendeleo, na aliwapatia zawadi ya Sh. milioni 10 kama pongezi kwa kazi yao nzuri.
Amesisitiza kuwa mawakala hao wamejitolea kwa hali na mali, kuhakikisha zoezi hilo linakamilika salama na kwa ufanisi, na kusimamia misingi ya 4R ya Rais Dr,Samia Suluhu Hassan.
“Mawakala wa CCM mmefanya kazi kubwa sana ya kusimamia zoezi hili na wananchi wameboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, na siku ya uchaguzi watatumia haki yao kidemokrasi kupiga kura,”amesema Katambi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amempongeza Katambi kwa kujali maslahi ya wananchi pamoja na kuunga mkono juhudi za chama, na kwamba katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu CCM watashinda kwa kishindo sambamba na uchaguzi mkuu mwakani 2025.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464