Header Ads Widget

WAZEE WAMTUMA MBUNGE CHEREHANI

WAZEE WAMTUMA MBUNGE CHEREHANI

Na Marco Maduhu, USHETU

BARAZA la ushauri la wazee halmashauri ya ushetu wilayani Kahama, wamewasilisha mahitaji na mapendekezo yao kwa mbunge wa jimbo la ushetu Emmanuel Cherehani, kuyawasilisha katika vyombo vinavyohusika na kufanyiwa utekelezaji kupitia nafasi yake ya ubunge.
Wazee wamewasilisha mahitaji na mapendekezo hayo leo Septemba 12,2024 kwa katibu wa mbunge wa jimbo la ushetu Elizabeth John, kwa niaba ya mbunge Emmanuel Cherehani.

Afisa ufuatiliaji masuala ya wazee kutoka baraza la ushauri la wazee mkoa wa shinyanga Laurent Mihayo, akiwasilisha mapendekezo hayo kwa niaba ya mwenyekiti wa baraza la wazee halmashauri ya ushetu, amesema wanamtuma mbunge huyo kuwasemea juu ya kuhuisha sera ya wazee (2003), ili ipate kutungiwa sheria na kupata nguvu ya kutekelezewa mahitaji yao kwa mujibu wa sheria.
Ametaja mapendekezo mengine ni wazee wanahitaji wawe wanapewa malipo ya pensheni kila mwezi, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, sababu wazee wachache wapo kwenye mfumo rasmi na wengine kwenye mifumo isiyo rasmi, na pia wazee wastaafu wa zamani waongezewe malipo ya pensheni kama ilivyo wastaafu wa sasa.

“Wastaafu wa nyuma kipindi cha hayati Rais Benjamini Mkapa, malipo ya pensheni yao yapo chini sana tofauti na wasasa, hivyo tunaomba na wao waongezewe ili kuendana na hali ya maisha ya sasa kutokana na vitu kuwa na gharama kubwa,”amesema Laurent.
Mapendekezo mengine ni ustawi wa jamii iwe idara inayojitegemea, pamoja na kuwa na bajeti ya kuratibu shughuli za wazee, pia wazee washirikishwe kwenye vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi za chini mpaka taifa ikiwamo kuwa na uwakilishi bungeni.

Wamesema pia kanuni za bima ya afya kwa wote ziwe jicho kwa wazee, na kuwatambua wazee kama wanufaika wa matibabu bila malipo, pamoja na kuwapo na sheria mahususi inayowabana watoto na jamii kuwatunza wazee ili kuepuka vitendo vya utelekezaji.
“Mapendekezo mengine ni mikopo inayotolewa kwa makundi maalumu asilimia 10 za halmashauri ambayo inaangazia zaidi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, tunaomba na wazee wanaume nao tuingizwe kwenye mpango huu sababu wapo wazee wenye nguvu ambao wanaweza kupata mkopo na kufanya shughuli za kuwaingiza kipato,”amesema Laurent.

“Sisi wazee tunatambua jitihada za dhati zinazochukuliwa na serikali na wadau wa maendeleo kwa ajili ya ustawi wetu, tuna tambua mchango wa viongozi na wawakilishi wa wananchi wakiwamo wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji,vitongoji, mitaa, watendaji na wataalamu wote, hivyo kupitia uwakilishi wa mbunge Cherehani, tunaomba mapendekezo yetu na mahitaji ayawasilishe kwenye vyombo vinavyohusika kwa ajili ya utekelezaji,”ameongeza.
Naye katibu wa mbunge Cherehani, Elizabeth John,amesema wazee ni dhahabu na kwamba mbunge anawapenda sana na kuwathamini, na hata baadhi ya mapendekezo ambayo wamemuwasilishia baadhi amesha anaza kuyasemea bungeni likiwamo suala la mikopo.

Amesema mapendekezo yao yana mashiko likiwamo pia suala la pesheni kwa wazee, sababu kwa sasa gharama za maisha zimependa, hivyo ongezeko la pesheni kwa wazee wastaafu wa zamani ni muhimu sana, huku akibainisha kwamba mapendekezo hayo atampatia mbunge na atayafanyia kazi na kuyafikisha sehemu husika.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Afisa ufuatiliaji masuala ya wazee kutoka baraza la ushauri la wazee mkoa wa shinyanga Laurent Mihayo, akiwasilisha mahitaji na mapendekezo ya wazee kwa katibu wa mbunge wa jimbo la ushetu Elizabeth John.
Afisa ufuatiliaji masuala ya wazee kutoka baraza la ushauri la wazee mkoa wa shinyanga Laurent Mihayo akikabidhi mahitaji na mapendekezo ya wazee kwa katibu wa mbunge Elizabeth John.
katibu wa mbunge wa jimbo la ushetu Elizabeth John akizungumza na wazee.
Picha ya pamoja ikipigwa.

Post a Comment

0 Comments