BUTONDO “FAMILY” WAUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA WAJENGA MRADI WA MAJI KWA FEDHA ZAO BINAFSI KUMTUA NDOO KICHWANI MWANAMKE
MBUNGE wa jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, ameungana na Dada yake Margareth Butondo ambaye anaishi nchini Ufaransa, kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kumtua ndoo kichwani mwanamke, kwa kuamua kujenga mradi wa maji kwa fedha zao binafsi katika kijiji cha Kisesa wilayani Kishapu.
Mradi huo wa maji ni wa kisima kirefu ambao tayari umeshaanza utekelezaji kwa hatua za awali za uchimbaji wa kisima kirefu (Butondo Water Project), na utakamilika ndani ya miezi mitatu ijayo na gharama zake itakuwa ni sh.milioni 27.
Mheshimiwa Butondo mbali na kufika kuona maendeleo ya ujenzi wa kisima hicho, pia alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Kisesa, Mkutano ambao umefanyika Mizanza mahali ambapo mradi huo wa maji unajengwa na kuhudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kishapu Boniphace Mwandu.
Amesema wananchi wa kijiji hicho wanashida kubwa ya maji, hivyo yeye na dada yake walijadili kuona namna ya kuwasaidia, ndipo wakaamua kutoa fedha zao binafsi, ili kumuunga Mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo kichwani mwanamke, na kuanzisha ujenzi wa mradi huo wa maji.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya muda mfupi amefanya mambo makubwa sana katika nchi hii likiwamo na jimbo la Kishapu, ametoa fedha na miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa ikiwamo ya maji, na sasa ametoa tena pesa kujengwa visima vya maji vitano vitano kwa kila jimbo, nani kama Samia”amesema Butondo,
“Kutokana na juhudi hizi ambazo anaonyesha Rais wetu Samia za kutatua changamoto ya ukosefu wa maji na kumtua ndoo kichwani mwanamke, ndipo mimi na dada yake Margareth Butondo, tukaona tumuunge mkono na kutoa fedha zetu binafsi kuanzisha ujenzi wa mradi wa maji wa kisima kirefu katika kijiji hiki cha Kisesa,”ameongeza.
Amesema baada ya kukamilika uchimbaji huo wa kisima cha maji, hatua za awali litawekwa bomba la kupampu maji ili wananchi waanze kuyatumia, na baadae litajengwa tenki kubwa la maji, ili kusambaza maji hayo kwa vitongoji vyote vya kijiji hicho cha kisesa, kwa kuweka vituo vya kuchotea maji kila mahali.
Aidha, amempongeza pia Rais Samia Suluhu Hassani kwamba katika Jimbo hilo amekuwa akitatua shida ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi, na awali alishajenga visima vya maji 12 na vinafanya kazi, na sasa yupo kwenye ujenzi wa vingine vitano ambavyo vinajengwa Kata ya Mwagembe, Somagedi,Mwaweja, Mwataga na Mwandu.
Amesema licha ya ujenzi wa visima hivyo vya maji, pia amepata miradi ya maji ya ziwa Victoria, na kwamba kabla hajawa Mbunge ni Kata tatu tu ndiyo zilikuwa na Maji hayo, ambazo ni Mhunze, Maganzo na Mwadui Luhumbo, lakini sasa hivi zaidi ya Kata 10 zina maji ya ziwa Victoria na miradi mingine bado inaendelea kutekelezwa.
Katika hatua nyingine Butondo amewaunga Mkono wananchi wa kijiji cha Kisesa, kwa kutoa kiasi cha fedha Sh.laki tano kwa ajili ya ukamilishaji wa marambo mawili ya maji ambayo waliyaanzisha kwa nguvu zao kwa ajili ya kunyweshea mifugo, huku akitoa maagizo pia kwa Mkuu wa idara ya mifugo na Kilimo wilayani humo Sabinus Chaula kushirikiana na wananchi kwenye ujenzi huo.
Katika hatua nyingine Butondo, ametaja miradi mingine ya maendeleo ambayo imetekelezwa wilayani humo ikiwamo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, Sekta ya elimu, umeme, Afya, na kwamba katika Afya vimejenga Vituo vya afya vipya Vitano, Zahanati 12 na Hospitali ya wilaya, na kuna vifaa tiba vya kisasa digital X-RY,CT-SCAN na upatikanaji wa madawa upo kwa asilimia 90.
Fundi Sanifu kutoka RUWASA wilayani Kishapu Alex Makono, ambao wameshiriki kufanya utafiti wa upatikanaji wa maji kwenye mradi huo, amesema wanaishukuru Familia ya Mbunge kwa kutatua changamoto hiyo ya ukosefu wa maji kijijini humo, na kwamba watashirikiana naye kwa kila hatua hadi kuukamilisha ikiwamo na kusambaza maji kwa kila kitongoji cha kijiji hicho.
Nao wananchi wa kijiji cha Kisesa, wamemshukuru Mbunge Butondo kwa kuguswa na matatizo ya wananchi, na kufikia hatua ya kutoa fedha zake binafsi kwa kushirikiana na Familia yake kutatua shida zao, na kwamba kijiji hicho wanashida kubwa ya maji, na kukamilika kwa mradi huo utawasaidia kuondokana pia na matumizi ya maji yasiyofaa.
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kishapu Boniphace Mwandu, amempongeza Mbunge Butondo, kwamba ni Mbunge mzuri sababu anajua matatizo ya watu, na amekuwa akipambana kuyatatua na hata kuyasemea Bungeni, ndiyo maana amehudhuria kwenye mkutano wake sababu ni mbunge ambaye anamkubali katika utendaji wake kazi, na habagui kuwapelekea wananchi maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu, amesema Jimbo hilo sasa limepata Mbunge, na amekuwa akiitendea vyema ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kushirikiana na Rais Dk,Samia Suluhu Hassan kutatua shida za wananchi wa Kishapu, ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa na imekuwa Kishapu mpya.
Aidha, amewasihi pia wananchi kwamba katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wale wenyesifa wanawake na vijana, wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi, na kwamba siku ya uchaguzi Novemba 27 watu wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi ambao watawaletea maendeleo.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akiangalia eneo ambapo kisima kirefu cha maji kimechimbwa.
Mtambo ukichimba kisima kirefu cha maji.
Maji yakitoka mara baada ya kisima kuchimbwa.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akizungumza na wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu akizungumza na wananchi kwenye mkutano.
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kishapu Boniphace Mwandu, akizungumza kwenye mkutano huo wa Mbunge Butondo.
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kishapu Boniphace Mwandu (kulia)akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo kwa kuwaletea maendeleo wananchi bila ya ubaguzi na hata kutoa fedha zake binfasi kutekeleza miradi ya maendeleo ukiwamo wa kisima kirefu cha maji kijiji cha Kisesa.
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kishapu Boniphace Mwandu (kushoto)akiendelea kumpongexa Mbunge Butondo.
Mkutano ukiendelea.
Ujenzi wa kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Kisesa wilayani Kishapu ambao unatekelezwa na Familia ya Mbunge Boniphace Butondo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464