BUTONDO AITEKA UKENYENGE


BUTONDO AITEKA UKENYENGE

Achangia mifuko 100 ya saruji ujenzi shule mpya ya wila

Na Marco Maduhu,KISHAPU
MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo,amefanya mkutano mkubwa wa hadhara Kata ya Ukenyenge jimboni humo, na kuelezea miradi ya maendeleo ambayo ameitekeleza ndani ya muda mfupi kwa kipindi cha miaka minne ya ubunge wake na kutatua kero nyingi za wananchi.

Amefanya mkutano huo wa hadhara jana na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa Ukenyenge, huku wakipongeza kazi kubwa ya maendeleo ambayo ameifanya chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na kuitendea vyema ilani ya uchaguzi ya CCM.
Butondo akizungumza na mamia ya wananchi wa Ukenyenge, amesema awali Kata hiyo hapakuwa na Kituo cha Afya, lakini kipindi kifupi cha ubunge wake sasa hivi kituo kipo, kikiwa na vifaa tiba vya kisasa pamoja na madawa ya kutosha.

Amewataka wananchi hao kwamba ili waendelee kunufaika na huduma za matibabu kwenye kituo hicho,wajiunge na bima ya afya CHF, ili watakapoungua wakiwa hawana pesa waweze kupata matibabu bure na kuokoa afya zao.
Amesema changamoto ambazo zipo kwenye kituo hicho cha afya likiwamo tatizo la ukosefu wa Genereta ya dharura na wodi za wanaume, kuwa suala hilo amelichukua na watalifanyia kazi haraka iwezekanavyo, ili huduma za matibabu ziendelea kutolewa vizuri kwa wananchi, kama ilivyo adhima ya Rais Dk.Samia ya kuimarisha afya za wananchi.

“Hapa Kata ya Ukenyenge chini ya Rais wetu Dk,Samia Suluhu Hassan, ndani ya muda wangu mfupi wa ubunge tumefanya mambo makubwa ya kimaendeleo, pamoja na kuleta mradi wa umeme wa Jua ambao utawanufaisha nyie na taifa kwa ujumla,”amesema Butondo.

Aidha, amesema awali hapo Ukenyenga kulikuwa na daraja finyu, lakini kilio hicho cha wananchi kilisikika na kujengwa daraja kubwa lenye thamani ya sh.bilioni 1.7, na pia barabara ambazo zilikuwa mbovu na kushindwa kupitika sasa hivi zinapitika, na kipindi anaingia kwenye ubunge 2020 mtandao wa barabara kishapu ulikuwa kilomita 670 na amefikisha kilomita 1,024.
“Niwaambie tu kwa upande wa barabara sasa hivi hakuna Kata ambayo haipitiki, na zile barabara ambazo zilikuwa mbaya na kero kwa wananchi ikiwamo ya Uchunga, Kiloleli na Itilima, sasa hivi ziko vizuri na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi bila shida ikiwamo kusafirisha mazao,”amesema Butondo.

Amezungumzia pia upande wa upungufu wa vyumba vya madarasa, kwamba kabla ya ubunge wake kwa shule za msingi kulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa asilimia 80 na Sekondari 75, lakini sasa hivi upungufu upo asilimia 15 kwa Msingi na Sekondari, na bado vyumba vya madarasa zinaendelea kujengwa yakiwamo na mabweni ya wasichana.
Amesema Serikali awamu ya Sita ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haina mchezo kwenye suala la elimu, ndiyo maana imekuwa ikitoa fedha ilikujengwa vyumba vya madarasa, kwa kuhakikisha madarasa na madawati yanakuwapo ya kutosha.

“Niwapongeze pia wananchi kwa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia, na hata kuanzisha ujenzi wa shule mpya ikiwamo shule ya Msingi Kitongoji cha Wila, na sasa mpo usawa wa renta na mimi nawaunga mkono kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji,”amesema Butondo.
Kwa upande wa maji, amesema kata hiyo sasa hivi ina maji ya kutosha, na kusalia kwenye vitongoji viwili vya Wila na Iwelemo, ambayo navyo katika mwaka huu wa fedha, vipo kwenye mpango wa kupelekewa huduma ya maji, huku akitoa wito pia kwa wananchi wavute maji majumbani mwao.

Suala la umeme, amesema upo wa kutosha kwenye Kata hiyo, na kwamba Novemba mwaka huu kuna mikataba inasainiwa ya kufikisha umeme kwa kila kitongoji, na pia katika jimbo hilo kuna minara 18 ya mawasiliano, na hakuna eneo ambalo halina mtandao tofauti na miaka ya nyuma.
“Kipindi naingia mimi kwenye ubunge, jimbo zima la Kishapu ni vijiji 40 tu vilikuwa na umeme, lakini sasa hivi kati ya vijiji 127 vimesalia viwili tu ndivyo havina umeme,Sanjo na Mwataga, kwa kifupi miradi mingi sana ya maendeleo tumeitekeleza kwa muda mfupi”amesema Butondo.

Amegusia pia suala la michezo kwa vijana, kwamba atawalepelekea mipira pamoja na jezi, hali ambayo itasaidia kuibua vipaji vya vijana hao.
Paroko wa parokia ya Wila wilayani Kishapu John Nkinga, akizungumza kwenye mkutano huo, amempongeza Mbunge Butondo kwa kazi kubwa ya maendeleo ambayo ameifanya, na kwamba wao kama watumishi wa Mungu wamekuwa wakifanya kazi zao za kutoa huduma kwa jamii bila shida kutokana na uboreshwaji wa miundombinu.

Nao wananchi wa Ukenyenge wamemtaka Mbunge huyo, kwamba aendelee kuchapa kazi ya kuwaletea maendeleo, na akaze uzi hivyo hivyo, kwa vile yeye ni Mwana Kishapu na anajua matatizo yao, hivyo wanamtegemea sana katika utatuzi wa kero zao.

TAZAMA PICHA CHINI👇👇
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Kata ya Ukenyenge.
Diwani wa Ukenyenge Anderson Mandia akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa viti maalum akizungumza kwenye mkutano huo.
Paroko wa parokia ya Wila wilayani Kishapu John Nkinga, akizungumza kwenye mkutano huo.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Wananchi wa Ukenyenge wakiwa kwenye mkutano hadhara.
Mkutano wa hadhara ukiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464