BUTONDO APELEKA FURAHA YA UMEME SHULE YA SEKONDARI MWAMASHELE

BUTONDO APELEKA FURAHA YA UMEME SHULE YA SEKONDARI MWAMASHELE

Na Marco Maduhu,KISHAPU

MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, ameahidi kuwapeleka huduma ya umeme katika shule ya Sekondari Mwamashele.
Butondo ametoa ahadi hiyo alipotembelea shule hiyo,kuona maendeleo ya shule pamoja na ujenzi wa bweni la wasichana shuleni hapo,na pia kuzungumza na wanafunzi na kuwasihi wasome kwa bidii.

Amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kimasomo, pamoja na kupata matokeo ya shule 10 bora, na hivyo kuahidi kuwapelekea huduma ya umeme, ili wapate muda mwingi wa kujisomea pamoja na kupewa majaribio ya mara kwa mara kupitia uzalishaji wa mitihani sababu umeme utakuwapo.
“Nitatumia jitihada zangu zote kuleta umeme hapa shuleni, sababu miundombinu ipo na tayari mmeshafanya “wirering”na haita fika Octoba lazima umeme uwepo hapa shuleni,”amesema Butondo.

“Umeme ukifika hapa shuleni utakuwa na faida kubwa sana sababu mtakuwa na Photocopy mashine na mtakuwa mkichapisha mitihani yenu hapa hapa shule yakiwamo majaribio, na hakuna tena kwenda Mhunze kuichapisha kwenye “stationary” za watu binafsi na kutumia gharama nyingi,” ameongeza Butondo.
Aidha, amesema umeme huo pia utakuwa ni fursa nzuri kwa wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea hata nyakati za usiku kwa wanafunzi ambao wanaishi jirani na shule.

Katika hatua nyingine Butondo, ameahidi kushirikiana kikamilifu kukamilisha bweni la wasichana shuleni hapo, na kwamba awali alishatoa mifuko 100 ya saruji.
Pia, akiwa katika shule hiyo aliahidi kuwapatia wanafunzi vifaa vya michezo, ikiwamo mipira pamoja na jezi.

Meneja wa TANESCO wilaya ya Kishapu Mhandisi Elias Turnbull, alipopigiwa simu na Mbunge kueleza ni lini atapeleka huduma ya umeme shuleni hapo, amesema kutokana na bajeti kuwapo ya shule hiyo haitapita mwezi Octoba umeme utawashwa katika shule hiyo.
Mkuu wa shule ya Sekondari Denis Fungo, amesema kupatikana kwa huduma ya umeme shuleni hapo utasaidia kuwapunguzia gharama hasa za uzalishaji mitihani, sababu hua wanatumia Sh.laki 7, lakini fedha za serikali ambazo wanapokea kila mwezi ni laki 3, na kwamba wakipata umeme shule hapo gharama zitapungua.

“Shuleni hapa tumeshafanya “wirering” tunasubili tu kuvutiwa umeme,”amesema Fungo.
Nao baadhi ya wanafunzi wa kike shuleni hapo,wamemshukuru Mbunge Butondo kwa kuonyesha jitihada zake za kuwakamilishia bweni, pamoja na kuwapambani kupatiwa huduma ya umeme, ambao utawasaidia katika masomo yao na kufanya vizuri zaidi, sababu watakuwa na muda mwingi wa kujisomea hadi nyakati za usiku.

 PICHA BWENI LA WASICHANA👇👇
Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo akikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la wasichana shule ya sekondari Mwamashele.
Muonekano wa bweni la wasichana shule ya Sekondari Mwamashele.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamashele wilayani Kishapu wakiwa na Mbunge wao Boniphace Butondo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464