BUTONDO KUPELEKA MIFUKO 100 YA SARUJI KU-“SUPPORT” UJENZI KITUO CHA AFYA BUBIKI,AFANYA MKUTANO MKUBWA WA HADHARA


Na Marco Maduhu,KISHAPU

MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, amefanya mkutano mkubwa wa hadhara kata ya Bubiki, na kuahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo cha Afya cha Kata hiyo,ambacho kimechukua miaka 12 kushindwa kukamilika.

Butondo ametoa ahadi hiyo leo  Septemba 24,2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Bubiki kwenye Mkutano wa dhadhara, na kuelezwa juu ya changamoto ya kushindwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Afya, ambacho kilianzishwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2012.
Amesema anafahamu ujenzi wa kituo hicho cha Afya, na kwamba hapo baada ya kuwa Mbunge 2020, awali alishawahi kutoa tena mifuko 100 ya saruji ili kuendeleza ujenzi wake, lakini kwa taarifa aliyopewa kwamba mifuko hiyo ilibadilishiwa matumizi, kwenda kumalizia ujenzi wa nyumba za Walimu shule ya Msingi Ushirika.

Amesema kutokana na kufahamu umuhimu wa huduma za Afya kwa jamii,hivyo ameamua kuchangia tena mifuko 100 ya saruji, ili kusukuma ujenzi wa Zahanati hiyo,huku akitoa angalizo kwamba mifuko hiyo isije na yenyewe tena ikabadilishiwa matumizi.
“Ujenzi wa kituo hiki cha Afya Bubiki sasa nalivalia njuga haiwezekani ujenzi uchukue muda hivyo kukamilika tangu mwaka 2012 na Kata hii ina watu wengi lakini hakuna huduma za afya lazima kikamilike,”amesema Butondo.

Mkurugenzi wa Kishapu Emmanuel Johnson, alipopigiwa simu na Mbunge Butondo, juu ya hatua ambazo Serikali imezichukua kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya Bubiki, amesema kwamba tayari walishaiombea bajeti yake serikali kuu, huku akisisitiza wakikwama kupata fedha hizo, mwaka ujao wa fedha wataitengea bajeti kupitia mapato ya ndani.
Afisa Kilimo Kata ya Bubiki Juma Magesa akisoma taarifa ya Kijiji kwa niaba ya Mtendaji wa kijiji, amesema wananchi Bubiki hawana huduma za Afya ambapo hupata matibabu kwenye Kata jirani ya Busangwa.

Amemuomba Mbunge huyo pamoja na Serikali, kusaidia kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Bubiki, ambacho kimechukua muda wa miaka 12 sasa kushindwa kukamilika na kusababisha wananchi kukosa huduma bora za matibabu.
“Ujenzi wa kituo hiki cha Afya Bubiki ulianza mwaka rasmi mwaka 2012 kwa nguvu za wananchi na sasa ipo usawa wa renta, tuna mshukuru Mbunge Butondo kwa kutuunga mkono hapo awali, ambapo alitupatia mifuko 100 ya saruji lakini ikabadilishiwa matumizi na kuelekezwa kwenye ujenzi wa nyumba za walimu shule ya msingi ushirika,”amesema Magesa.

Diwani wa Bubiki James Kasomi, amesema Kata hiyo ina jumla ya wananchi elfu 15, na kwamba wanatumia Zahanati moja ya Nyasamba kupata huduma tena ina watumishi watatu tu, na kumuomba Mbunge pamoja na serikali, kusaidia kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha Afya Bubiki ili kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Nao baadhi ya wananchi wa Bubiki,wamesema kukosekana na huduma za Afya wamekuwa wakipata shida ya kupata matibabu kwenda kwenye Kata za jirani.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akizungumza na wananchi wa Bubiki kwenye mkutano wa hadhara.
Katibu wa siasa na uenezi CCM wilaya ya Kishapu Jiyenze Seleli akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Bubiki James Kasomi akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Kilimo Kata ya Bubiki Juma Magesa akisoma taarifa ya Kijiji kwa niaba ya Mtendaji wa kijiji.
Wananchi wa Bubiki wakiwa kwenye mkutano wa Mbunge Boniphace Butondo.
Awali wananchi wa Bubiki wakimpokea Mbunge Boniphace Butondo alipowasili kuzungumza nao kwenye mkutano wa hadhara.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464