KATAMBI ATANGAZA MVUA YA MABILIONI YA DR. SAMIA SEKTA YA AFYA NA FURSA ZA MASOMO NA AJIRA


KATAMBI ATANGAZA MVUA YA MABILIONI YA DR. SAMIA SEKTA YA AFYA NA FURSA ZA MASOMO NA AJIRA

Na. Mwandishi wetu: Dodoma


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe.Jenista J Mhagàma, amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh. Bilioni tisa kwa ajili ya kusomesha Madaktari bingwa na Madaktari bingwa wabobezi nchini.


Mhe. Katambi ametoa pongezi hizo leo Septemba 26, 2024 jijini Dodoma katika Uzinduzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambao ulikuwa na kauli mbiu isemayo 'Utoaji wa Huduma za Afya Nchini Tanzania, Vipaumbele, Ushirikishwaji wa Wadau na Uendelevu'.


Aidha, amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika kuboresha huduma za matibabu ya kibigwa na ubigwa bobezi umeongeza idadi ya wagonjwa kutoka nje wanaokuja kutibiwa nchini kutoka 5,705 mwaka 2022 hadi 7,843 mwaka 2024.


Amesema serikali imeendelea kuhakikisha sekta ya afya inakua na kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za Afya ambavyo vimeongezeka kutoka vituo 8,549 Mwaka 2021 hadi vituo 9,693 Mwaka 2024.


Mhe.Katambi ametoa wito kwa watumishi wa sekta ya afya nchini kuweka utaratibu wa kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kutoa huduma bora kwa wananchi.


Pia mkutano huu umehudhuriwa na maprofesa, madaktari bingwa na wabobevu, RMOs na DMOs zaidi ya 325 kutoka nchi nzima
Awali, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Marko Hingi amesema Wizara imeendelea kufadhili wanafunzi na wataalam wa afya katika kada mbalimbali za kitabibu ili kuwa na ujuzi wa kutosha wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.


Naye, Rais wa Chama cha Madaktari (MAT) Dkt. Deus Ndilanha, ameiomba serikali kutoa kipaumbele cha ajira kwa kada ya afya ili kupunguza changamoto ya ajira iliyopo.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464