Header Ads Widget

WAUGUZI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MAADILI NA MIONGOZO YA UTUMISHI WA UMMA

Na George Mganga,

SHINYANGA RRH

WAUGUZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga wamekumbushwa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na miongozo ya Utumishi wa Umma ili kuboresha huduma nzuri kwa wateja.

Hayo yamesemwa Septemba 18, 2024 na Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali, Bi. Agnes Masesa, katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Akielezea umuhimu wa kuzingatia miongozo pamoja na huduma nzuri kwa mteja, Masesa aliwaomba wauguzi kuzingatia zaidi miongozo pamoja na maadili ya kazi, ili kukidhi matakwa makubwa ya wateja ambao wanapaswa kupewa huduma bila ubaguzi.

“Najua tunakutana na wagonjwa wengi, wengine wanakuja wakiwa na changamoto mbalimbali au hawako kwenye hali nzuri, isitupelekee sisi tukawa na hasira ya kuwajibu vibaya, tuwajibu vizuri na kwa kuwajali bila kuonesha ubaguzi wowote.

“Tujikite zaidi katika kuzingatia maelekezo ya Utumishi wa Umma yanavyotaka ili kuilinda pia taswira nzuri ya Hospitali na Serikali kwa ujumla, sababu itatusaidia kutengeneza imani nzuri kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu, Beatrice Gwakisa Cheyo, alisisitiza kwa kuwataka watumishi wote kuwa na lugha nzuri kwa wateja pamoja na kuzingatia miongozo.

Bi. Cheyo alieleza kuwa matumizi mazuri ya lugha kwa wateja yanawafanya wapatwe na faraja na kuona umuhimu wa huduma ambazo zinatolewa na Hospitali, lakini vilevile kutengeneza mazingira mazuri kwa wao kurejea tena Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga kwa ajili ya kupata huduma.

Kikao hicho kimekuwa ni sehemu ya vikao vya kila mwezi, ambavyo hufanyika kwa wauguzi ili kukumbushana masuala mbalimbali ya kazi zao, ikiwemo maadili ya utumishi na mawasiliano mazuri kati yao na wateja.

Post a Comment

0 Comments