MBUNGE BUTONDO AENDELEA KUCHANJA MBUGA,WANANCHI WAPAGAWA NA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

MBUNGE BUTONDO AENDELEA KUCHANJA MBUGA, WANANCHI WAPAGAWA NA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

Na Marco Maduhu,KISHAPU
MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo,ameendelea kufanya mikutano ya hadhara jimboni kwake,na kuelezea namna alivyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza leo Septemba 20,2024 na wananchi wa Mwamashele katika Mkutano wa hadhara, amesema ndani ya miaka yake minne ya ubunge, amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo na kuibadilisha wilaya ya kishapu, chini ya Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika Kata ya Mwamashele fedha nyingi zimetolewa za utekelezaji miradi ya maendeleo, zikiwamo na za mfuko wa jimbo, na kuboresha sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu,miundombinu ya barabara,afya,kilimo,umeme na maji.

Akizungumzia upelekaji wa maji ya ziwa victoria Mwamashele, kilio ambacho ni kikubwa kwa wananchi, amewahidi wananchi hao kwamba ndani ya mwezi mmoja au miwili wataanza kutumia maji hayo, na kwamba kuna mradi wa bilioni 6 ambao unatekelezwa utatoka Igaga kupita Mwamashele hadi Lagana tayari taratibu za manunuzi zilishaanza.
“Katika jimbo hili la Kishapu tunataka maji haya ya ziwa Victoria yasambae katika maeneo yote, na tunatekeleza kwa awamu awamu, na hali ya upatikanaji wa maji katika jimbo hili tumefikia asilimia 70, awali kabla sijawa mbunge ilikuwa asilimia 30, na changamoto hii ya tatizo la maji tunakwenda kuimaliza kabisa,”amesema Butondo.

Kwa upande wa umeme, amesema licha ya umeme kuwepo Mwamashele lakini haujasambaa maeneo mengi, serikali chini ya Rais Dk. Samia, imeongeza nguzo 40 ambazo zitasaidia kufikisha umeme sehemu kubwa, na kwamba mwezi Novemba kuna mikataba itasainiwa ya kusambaza umeme kila kitongoji.
Kuhusu barabara, amesema vijiji vingi vya Kishapu vimeunganishwa na barabara, na kwamba kabla hajawa mbunge kulikuwa na mtandao wa barabara kilomita 670, lakini ndani ya miaka yake minne ya ubunge, sasa hivi mtandao wa barabara ni kilomita 1,024.6.

“Utendaji wa kazi zangu mimi ni kuacha alama, hata nilivyokuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu nimeacha alama ya jengo la utawala lile ghorofa, nyie endeleeni kuniamini, mimi Kishapu naijua vizuri ni mtoto wenu sita waangusha lazima niwaletee maendeleo,”amesema Butondo.
Mhandisi wakala wa maji vijijini (RUWASA)wilaya ya Kishapu Mhandisi John Lugembe, akizungumza kwenye mkutano huo, amesema wiki ijayo watafika Mwamashele kwa ajili ya kufanya tathimini ya kupeleka maji ya ziwa Victoria, na kwamba hatua ya awali wataanza na ukarabati wa tenki la maji, ya pili ni kuingiza maji kwenye tenki hilo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Nao wananchi wa Mwamashele, wamempongeza mbunge Butondo kwa kuwaletea maendeleo, na kwamba hawakutegemea kama ipo siku watapata huduma ya umeme, lakini sasa hivi umeme upo licha ya kutofika maeneo mengi na wameahidiwa tena kupelekewa maji ya ziwa voctoria, kitendo ambacho wamedai kupagawa kuwa na mbunge mpenda maendeleo na kujali shida za wananchi.
Mmoja wa wananchi hao Elizabeth Dulushi, amesema hawakutarajia kama mbunge Butondo anaweza kufanya mambo makubwa kiasi hicho, kutokana na maneno maneno ya wanasiasa, lakini amejionea mwenyewe jinsi miradi ya maendeleo ilivyotekelezwa na kugusa kila sekta.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akizungumza na wananchi wa Mwamashele.
Diwani wa Kata ya Mwamashele Lucas Nkende akizungumza kwenye mkutano huo.
Mtendaji wa Kata ya Mwamashele Lilian Sixbert akisoma taarifa ya Kata kwenye mkutano huo.
Mtendaji wa kijiji cha Mwamashele Isack Samson.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akisalimia na wananchi wa Mwamashele.
Wananchi wa Mwamashele wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge Butondo.
Wananchi wa Mwamashele wakimpongeza Mbunge Butondo.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464