ALIYETUHUMIWA KUMTOBOA MACHO MTALAKA WAKE AKAMATWA

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari 

Suzy Butondo, Shinyangapress blog

Kufuatia tukio lililotokea Agosti 13 mwaka huu huko kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga juu Binti aliyefahamika kwa jina la Esta Mataranga (25) mkazi wa wilayani Shinyanga kutobolewa macho na aliyekuwa mme  wake aliyefahamika kwa jina la Paul Shija (19) na kisha kutokomea pasipojulikana  jeshi la polisi mkoani Shinyanga limedhibitisha kumkamata kijana huyo na kumuweka chini ya ulinzi.

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP. Janeth Magomi akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake amesema mnamo Septemba 17, 2024 walifanikiwa kumtia mbaroni Paul Shija mara baada ya kupokea taarifa fiche kutoka kwa wananchi, ambapo taratibu za kiupelelezi na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria zinaendela.

"Jeshi la polisi liliendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wananchi na Septemba 17, 2024 tulifanikiwa kumtia mbaroni maeneo ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga na kumfikisha kituoni na taratibu za upelelezi ukikamilika atachukuliwa hatua za kisheria", amesema Magomi.

Aidha kamanda Magomi ametoa onyo kwa wale wote wanaotenda uhalifu wakidhani wanaweza kukimbia na kujificha pasipo kukamatwa na jeshi hilo kuwa waachane na dhana hiyo kwani  jeshi hilo lina mkono mrefu na linafanya kazi katika maeneo yote huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikina na jeshi hilo katika kudhibiti uhalifu ili jamii iwe salama.

Katika hatua nyingine kamanda Magomi amekemea tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi pindi inapotokea kutoelewana na badala yake wafike katika vyombo vya sheria ili kuepukana ns vitendo kama hivyo .

"Tunaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kwamba waendelee kutoa taarifa za uharifu na wahalifu, kwani hata matokeo ya kumkamata huyu mtuhumiwa zimetokana na ushirikiano wa wananchi, hivyo tunawashukuru sana kwa kutoa taarifa hizi"amesema Magomi.

Baadhi ya wananchi Mariam Nkwabi amelishukuru sana jeshi la polisi kwa kuendelea kumfuatilia mharifu mpaka amepatikana, na sheria zifuate mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine.








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464