Header Ads Widget

MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA SHINYANGA KUANZA KUSIKILIZA KESI YA WACHIMBAJI WADOGO


Baadhi ya wachimbaji wadogo waliohudhulia mahakamani wakiwa kwenye picha ya pamoja  baada ya kutoka mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga

Suzy Butondo, Shinyangapress blog

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imetupilia mbali pingamizi la
kumkataa Jaji anayesikiliza kesi ya wachimbaji wadogo 18 wa madini ya dhahabu waliyoifungua wakidai fidia baada ya kufukuzwa kwenye machimbo ya dhahabu ya Imalamate wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Wachimbaji hao waliweka pingamizi la kumkataa Jaji Seif Kulita anayesikiliza kesi yao ya msingi inayohusu madai hayo ya fidia baada ya kufukuzwa kwenye machimbo ya dhahabu walikokuwa wakiendesha shughuli za uchimbaji wa dhahabu.

Mlalamikiwa katika kesi hiyo ni Rais wa Chama cha wachimbaji wadogo wa madini Tanzania (FEMATA) John Bina ambaye wanadai kwa sasa ni mmoja wa wamiliki wa machimbo hayo na kwamba baada ya kufukuzwa kwenye machimbo hayo walipoteza mali zao nyingi ikiwemo vifaa vya uchimbaji vilivyofukiwa kwenye maduara.

Msingi wa kumkataa Jaji Kulita ni baada ya kuona kesi yao imechukua muda mrefu kusikilizwa na kila tarehe ya kusikilizwa inapopangwa wamekuwa wakipigwa danadana na kesi huhairishwa pasipo sababu za msingi na wakati mwingine makarani ndiyo huwapa taarifa juu ya kesi kuahirishwa badala ya Jaji au Msajili wa Mahakama.

Katika hukumu yake juu ya pingamizi la kumkataa Jaji Kulita amesema sababu ambazo zimetolewa zote hazina mashiko na kwamba yeye ataendelea kuisikiliza, huku akiwataka walalamikaji kufanya marekebisho kwenye Hati yao ya madai baada ya wenzao wawili kujitoa kwenye kesi hiyo.

Baada ya kutupilia mbali pingamizi hilo Jaji Kulita amemwagiza mwanasheria upande wa walalamikaji awasilishe Mahakamani hapo Hati mpya ya madai mnamo Septemba 26 mwaka huu ambayo itakuwa imeondolewa majina ya Victor Batule na Mzee Ally ikiwa ni pamoja na gharama zao.

Pia Wakili wa mlalamikiwa apewe nakala ya hati hiyo ambayo atatakiwa kuijibu mnamo Oktoba 10 mwaka huu na Oktoba 17, 2024 wakili wa upande wa walalamikaji atajibu hoja za upande wa mlalamikiwa na kesi hiyo itatajwa au kusikilizwa mnamo Oktoba 21, 2024.

Awali wachimbaji hao walilalamikia kitendo cha kesi yao kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa hali ambayo wanahisi kuwepo mchezo mchafu unaotaka kufanywa na upande wa mlalamikiwa kutaka kufifisha kesi hiyo na kusababisha wenzao wengine kuanza kujitoa baada ya kurubuniwa.

"Kwa kweli tunasikitishwa na kitendo cha kesi yetu kupigwa danadana, maana tumeifungua mwaka jana mwezi Desemba, 2023 lakini mpaka leo hii tunapigwa tarehe kila siku, tunaingia gharama za usafiri na hali zetu kwa sasa ni ngumu kutokana na kutokuwa na kazi zozote za kufanya,"wamesema wachimbaji hao.

"Kibaya zaidi wakili wetu anatokea Dar es Salaam, hivyo kila mara tunaingia gharama za kumsafirisha kuja na kurudi, na mpaka sasa hatufahamu kesi hii itaanza kusikilizwa lini, ndo maana tuliamua kuweka pingamizi la kumkataa," ameeleza Jumanne ambaye ni mwenyekiti wa wachimbaji hao wadogo wa dhahabu.

Wachimbaji hao wamefungua kesi hiyo dhidi ya Rais wa FEMATA, John Bina wakidai alifanya ujanja wa kuwaondoa kwenye machimbo yao baada ya kufungwa kwa muda na Serikali ilipotokea ajali ya maduara kutitia na baadhi ya watu kupoteza maisha.

Mwenyekiti wa wachimbaji hao Jumanne Jembe Guguye amesema baada ya tukio hilo Serikali iliagiza machimbo kufungwa kwa muda huku ikitoa maelekezo kwa Ofisa madini kuweka mazingira mazuri yenye usalama na wachimbaji waendelee na shughuli zao lakini hata hivyo katika hali ya kutatanisha Bina aliwatangazia wachimbaji kwamba wanatakiwa kuondoka kabisa na wakafukuzwa kwa mtutu wa bunduki.

"Kutokana na hasara tuliyoipata tumeona tufungue kesi ya kumdai fidia John Bina ili atulipe shilingi zaidi ya bilioni moja kama fidia ya hasara aliyotusababishia na tunashangaa yeye ni Rais wa wachimbaji wadogo hapa nchini, sasa badala ya kutusaidia amegeuka kuwa mtu wa kutukandamiza," ameeleza Guguye

" Jumla ya fedha tunazomdai Jonh Bina ni shilingi Bilioni 1.8 na gharama za usumbufu jumla kuu shilingi Bilioni 3."ameongeza mwenyekiti Guguye
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Jumanne Jembe Guguye akizungumza
Mmoja wa wachimbaji hao akizungumza baada ya kutoka mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga
Mmoja wa wachimbaji hao akizungumza baada ya kutoka mahakama ya Tanzania kanda ya Shinyanga
Wachimbaji wadogo baada ya kutoka mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga
Wachimbaji wadogo baada ya kutoka mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga wakijadiliana jambo
Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga

Post a Comment

1 Comments