RC MANYARA AHAMASISHA WANANCHI KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA

 



Na Jaliwason Jasson, MANYARA

MKUU wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na vyama vya siasa ameongoza matembezi ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuboresha taarifa zao na kupata nafasi ya kupiga kura.

Sendiga ameongoza matembezi(Jogging)hayo  leo Septemba Mosi kuanzia  saa 12 asubuhi  ambayo yalianzia Uwanja wa Kwaraa na kumalizikia Uwanja huo.

Akizungumza mara baada ya matembezi hayo yaliyoshirikisha wabunge, katibu Tawala wa mkoa,  mkuu wa wilaya ya Babati, wakuu wa idara na vitengo, viongozi wa vyama vya  siasa, wenyeviti wa Halmashauri, wakuu wa taasisi za umma na binafsi, wafanyakazi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited na wananchi amewaomba wanawake na vijana kujitokeza kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ukifika.

Ametumia fursa hiyo ambayo ameipa jina la Daftari Day ili kutoa hamasa kwa wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu kuanzia Septemba 4 hadi  10.
Aidha amewaomba viongozi wa vyama vya siasa wahamasishe wanachama wao kujiandikisha ili ile Demokrasia wanayoitaka waweze kuipata na kwenda kupiga kura kwenye uchaguzi.

Amesema waliohama kutoka mikoa mingine, wilaya au kata amewataka kwenda kuboresha taarifa zao.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi akizungumzia zoezi hilo amesema mtu asipojitokeza kugombea nafasi za uongozi ataongozwa na mtu ambaye hamtaki au asiyekidhi vigezo.

Mulokozi amesema wao wanashiriki matukio ya kijamii kwa kuwa wanaohusika nayo ndio wateja wao wa vinywaji vikali.

Mkurugenzi huyo ametumia nafasi hiyo kuomba Tume Huru ya Uchaguzi(INEC) kuwawekea kituo cha kujiandikisha kiwandani kwao ili wafanyakazi iwe rahisi kupata nafasi.

Amesema wafanyakazi wake atawawekea mkakati wa kila mtu kujiandikisha anapotoka kazini ili asikose haki yake.
Pia mbunge wa vijana Taifa Hasia Halamga amesema vijana ambao walikuwa hawajajiandikisha walikuwa hawajafikisha miaka 18 wajiandikishe ili waweze kupiga kura na ni haki yao kikatiba.

Kwa upande wake Kaimu katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Manyara John William amewataka vijana kujitokeza kujiandikisha kwa wingi bila kuangalia Chama ili wapate haki ya kupiga kura.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464