RC MACHA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MIKATABA 33 YA MATENGENEZO YA BARABARA YA SH.BILIONI 10.27
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, ameshuhudia utiaji saini mikataba 33 ya matengenezo ya miundombinu ya barabara, baina ya wakandarasi na wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoani humo yenye thamani ya sh.bilioni 10.27.
Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo 33 imefanyika leo Oktoba 4,2024 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa shinyanga.
Macha akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi mkoani humo na kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akiwataka wakandarasi, kwamba miradi hiyo waitekeleze kwa uzalendo,weledi na ubora unaotakiwa, ili kuendana na thamani ya fedha “value for money.”
Amesema barabara ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu katika shughuli zake mbalimbali ikiwamo na kukuza uchumi, na kuwasihi wakandarasi wajitume kufanya kazi,na kwamba katika utekelezaji wa miradi hiyo waitekeleze wenyewe kupitia makampuni yao, na siyo kwenda kuwapatia watu wengine ambao hawana uwezo na kuharibu kazi hiyo.
“Msiende kugawa kazi hizi kwa watu wengine,nendeni mkazifanye wenyewe kama milivyoomba kupitia makampuni yenu, tunataka barabara hizi na madaraja yatengenezwe kwa ubora unaotakiwa,na mimi nitakuwa nafanya ziara ya kuzikagua,”amesema Macha.
Aidha,amewataka pia wakandarasi kwamba wanapokuwa wakitekeleza miradi hiyo washirikishe wananchi wa maeneo husika, pamoja na kuwapatia ajira zisizo hitaji ujuzi mkubwa, kutoa mikataba sahihi na kuwalipa kwa wakati.
Amewasisitiza pia wanapochimba udongo na changalawe wazingatie taratibu na kutochimba kando ya barabara, na kuwasihi pale malipo yao yanapochelewa wawe wavumilivu wakati serikali ikiendelea kuwashughulikia, na kwamba katika uandishi wa mabango ya kutambulisha miradi waandike kwa lugha ya kiswahili.
Awali Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Avith Theodory, akisoma taarifa amesema,wakandarasi walioshinda zabuni za matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja ni 21,na mikataba ambayo ina sainiwa ni 33, yenye thamani ya sh.bilioni 10.2.
Amesema matengenezo hayo ya barabara yanatumika kwa vyanzo vya fedha za mfuko wa barabara, tozo za mafuta pamoja na mfuko wa jimbo,na barabara ambazo zitafanyiwa matengenezo ni urefu wa kilomita 716.64, ujenzi wa makalvati 381,madaraja 4,mitaro urefu wa mita 5,280, pamoja ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilomita 2.8 na uwekaji wa taa za barabarani.
“Wakandarasi waliopatikana ni kutoka mikoa mbalimbali wakiwamo wenyeji wa mkoa huu wa shinyanga,wamepatikana baada ya kutangaza kazi hizi kupitia mfumo wa kielekitronik wa manunuzi (NesT) mwanzoni mwa mwezi was aba,”amesema Mhandisi Theodory.
“Tumetumia muda kidogo kuwapata pasipo kawaida kwani ililazimika kuuliza ili kupata udhibitisho wa tabia na sifa za utendaji kazi wao katika mikoa mingine walipowahi kufanya kazi, hivyo tunaamini kabisa watakwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba ili kufikia malengo kusudiwa,”ameongeza.
Mmoja wa wakandarasi kutoka kampuni ya Gapro Construction Limited Mhandisi Amedeus Mselle,ameishukuru Serikali kwa kuwa amini wakandarasi wazawa, na kwamba watafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa na kukamilisha kwa wakati.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akishuhudia utiaji saini mikataba ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 baina ya Wakandarasi na TARURA.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464