Header Ads Widget

MPAKA SASA HAKUNA KASORO TULIYOIBAINI KATIKA UJENZI HUU - MHE. NDEJEMBI

MPAKA SASA HAKUNA KASORO TULIYOIBAINI KATIKA UJENZI HUU - MHE. NDEJEMBI

Na. Paul Kasembo, Msalala

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema baada ya kutembelea shule ya sekondari Ntobo hakuna kasoro waliyoibaini katika ujenzi huu wa Shule hiyo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, huku akipongeza zaidi kwa kubakia na salio.

Mhe. Ndejembi amesema haya leo Oktoba 6, 2024 alipofika shuleni hapo kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili mkoani Shinyanga.

"Nawapongeza sana Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hii ya Ntobo, tumetembelea, tumekagua lakini mpaka sasa hakuna kasoro tuliyoiona katika utekelezaji wa mradi huu zaidi ya yote shule inao ubora unaoendana na thamani ya pesa na kwamba mmebakiwa na zaidi ya Mil. 10 huu ni mfano wa kuigwa," amesema Mhe. Ndejembi.

Akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Ntobo Sekondari Mwl. Hussein Mbwambo amesema kuwa wanayo furaha kumtaarifu Waziri kuwa ujenzi wa madarasa 7, matundu 8 ya vyoo, ofisi 1 ya walimu umekamilika vizuri na kubakiwa na salio la zaidi ya Sh. Milioni 10 ambapo wamemuomba Mkurugenzi wa Msalala awaruhusu zitumike kukarabati jengo la utawala.

Kwa upande wake RC Macha amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia fedha za miradi ya maendeleo katika Mkoa huu ambapo katika Sekta ya Elimu zimeboresha miundombinu yote muhimu ya watu wenye ulemavu, ya kufundishia walimu na kusomea wanafunzi jambo ambalo limekuja kuondoa tofauti ya Shule za binafsi na za Serikali kwani kwa sasa shule zinavutia zaidi kuliko za binafsi.

Ujenzi wa Ntobo Sekondari ulianza mwaka 2006, ni shule ya kutwa ambayo ni mchanganyiko ambayo kwa sasa ina Kidato cha kwanza hadi cha nne na jumla ya wanafunzi 577 sanjari na bweni la watoto wa kike lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 48.

Katika ziara hii, Mhe Ndejembi ameongozana na mwenyeji wake Mhe. Macha, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita, Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Iddy Kassim na wataalam mbalimbali ambayo itakamilika kwa mkutano wa hadhara Kata ya Segese.

Post a Comment

0 Comments