RC MACHA AJIANDIKISHA DAFTARI LA WAKAZI

RC Macha ajiandikisha daftari la wakazi

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amejiandikisha kwenye daftari la wakazi, huku akionya kuandikisha watu ambao siyo Raia wa Tanzania.

Amejiandikisha leo Oktoba 12,2024 kwenye viwanja vya Ikulu Manispaa ya Shinyanga, akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.

Macha akizungumza mara baada ya kujiandikisha kwenye daftari hilo, ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha, ili wapate fursa ya kupiga kura Novemba 27 na kuchagua viongozi wazuri ambao watawaletea maendeleo.

"Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan jana amejiandikisha kwenye daftari la wakazi, na mimi nimejiandikisha leo, naomba wananchi nao wajitokeze kwa wingi kujiandikisha, ambapo zoezi hili litakwenda hadi Oktoba 20,"amsema Macha.

Aidha,ameagiza kamati ya ulinzi na usalama,maofisa uandikishaji pamoja na Jeshi la uhamiaji,kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa kina ili kutoandikisha watu ambao siyo Raia wa Tanzania.

Ametoa wito pia kwa wananchi wenye sifa, kwamba wajitokeze kuwania nafasi za uongozi wakiwamo vijana na wanawake.

Amesema katika Mkoa wa Shinyanga watu ambao wanatarajiwa kupiga kura ni Milioni 1.1 na vituo vilivyopo vya uandikishaji ni 2,941.

Mmoja wa wananchi ambaye amejitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wakazi Magret Mapela, amesema amejiandikisha ili apate fursa ya kupiga kura na kuchagua viongozi waadilifu ambao watawaletea maendeleo.

Wakala wa Chadema Said Kibuya amesema zoezi hilo la uandikishaji lina kwenda vizuri,huku akisisitiza hamasa iongezwe zaidi ili wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari hilo la wakazi.

zoezi la uandikishaji datfari la wakazi kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa lilianza Jana Oktoba 11 na litakwenda hadi tarehe 20.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akijiandikisha kwenye daftari la makazi
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464