WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAPEWA MAFUNZO JUU YA SHERIA MPYA YA UNUNUZI WA UMMA NA PPRA

WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAPEWA MAFUNZO JUU YA SHERIA MPYA YA UNUNUZI WA UMMA NA PPRA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WAANDISHI wa habari mkoani Shinyanga,wamepewa mafunzo ya kufahamu sheria mpya ya ununuzi wa umma namba10 ya mwaka 2023.
Mafunzo hayo yametolewa leo Oktoba 23,2024,na Mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma (PPRA) kwa kushirikiana na Klabu ya uandishi wa habari mkoani Shinyanga.

Mwakilishi wa Meneja ya Kanda ya Kati kutoka PPRA Alfred Nicodemus, amesema mafunzo hayo wameyatoa kwa waandishi wa habari, ili wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao hasa katika uandishi wa habari za manunuzi,waandike kwa usahihi na kuhabarisha umma kitu sahihi.
Amesema manunuzi ya umma yana husisha fedha ambazo ni kodi za wananchi,hivyo habari ambazo zitaandikwa za manunuzi ya umma zinapaswa ziwe na usahihi na kutoleta taharuki.

"asilimia 70 hadi 80 ya pato la taifa,imeelekezwa kwenye manunuzi ya umma,"amesema Nicodemus.
Aidha,amesema kazi ya PPRA moja wapo ni kuhakikisha katika manunuzi ya umma, ikiwamo kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ni kuona thamani halisi ya fedha inaonekana "value for money"

Ametaja sababu za mapendekezo ya kutungwa kwa sheria hiyo mpya ununuzi wa umma, kuwa ilitokana na bei kubwa ya bidhaa,huduma na kandarasi ikilinganishwa na bei ya soko, kukosekana kwa viwango vya ukomo wa uidhinishaji wa zabuni.
Sababu zingine ni usimamizi hafifu wa masuala ya mnyororo wa ugavi,kutofungamanishwa na ununuzi katika sheria,matumizi mabaya ya utaratibu wa “Force Account” katika utekelezaji wa miradi,usimamizi hafifu wa mikataba ya ununuzi kutokana na ukosefu wa masharti mahususi katika sheria za usimamizi wa mikataba.

zingine ni sheria kutotofautisha masharti ya ununuzi kati ya taasisi za umma zinazojiendesha kibiashara,sheria kutoa mwanya wa ununuzi kutekelezwa nje ya mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki,na kusababisha matumizi hafifu ya mfumo, kutokuwepo kwa sharti la bei kikomo katika ununuzi wa umma.
Ameongeza kuwa sababu zingine ni sheria kutokuwa na masharti ya ukomo wa thamani ya miradi, muda mrefu katika utekelezaji wa michakato ya ununuzi, kutotolewa kwa adhabu mara ya pili kwa kosa moja kwa wazabuni waliofungiwa nje ya nchi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, amesema manunuzi ya umma yakikosewa yanaweza kuliingiza taifa kwenye mgogoro mkubwa, huku akiwasihi waandishi wa habari, kwamba pale watakapo kwama wanapokuwa wakiandika habari za manunuzi wasisite kuwasiliana mamlaka husika au PPRA, ili habari yao waiandike kwa usahihi na kutopotosha umma, na hata kukiingiza chombo chake kwenye matatizo.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Shinyanga Patrick Mabula, akisoma taarifa kwa niaba ya Mwenyekiti Greyson Kakuru,amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari, ili kuelewa zaidi mifumo ya sekta ya manunuzi.

"Warsha hii ni muhimu kwa waandishi wa habari,ili kuelewa zaidi juu ya mifumo ya sekta ya manunuzi, na kudhibiti rushwa,kurahisisha mchakato wa zabuni kwa uwazi kwa maofisa manunuzi, kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi,”amesema Mabula.
Nao baadhi ya waandishi wa habari, wamesema mafunzo hayo yatawasaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yao,na kuandika habari kwa usahihi za manunuzi ya umma.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga Patrick Mabula akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo ya PPRA yakiendelea.









Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464