Na Marco Maduhu,SHINYANGA
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga,limekamata jumla ya watuhumiwa 14 wakijihusisha na vitendo mbalimbali vya kihalifu, huku likionya watakao tishia kuvuruga amani uchaguzi serikali za mitaa watashughulikiwa kisheria.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kennedy Mgani, amebainisha hayo leo Oktoba 23,2024 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Amesema kwa kipindi cha kuanzia Septemba 26 hadi Oktoba 22 mwaka huu, wamefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 14 wakiwa pamoja na vielelezo mbalimbali.
Ametaja vielelezo ambavyo wamevikamata kuwa ni pombe ya moshi lita 87 na mitambo miwili ya kutengenezea pombe hiyo, Tv 3,decoder 1,Antena 1,meza 2 na viti 6 vya plastiki,pikipiki 5,drill mashine 2,rooter 1,hardisk 1,Betri 2 za solar,invetor 1 na godoro 2.
"Katika vielelezo hivi vyote watuhumiwa 14 tunawashikilia na upepelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria," amesema Mgani.
Aidha, amesema kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, wamekamata jumla ya magari 3,358, bajaji na pikipiki 1,027 na kwamba wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini ya papo kwa papo, huku dereva mmoja wakimfungia lessen kipindi cha miezi mitatu.
Amesema jeshi hilo pia limekuwa likitoa elimu na sasa limezindua kampeni ya "Tuwaaambie kabla ya hawajaharibiwa" ikiwa na lengo la kufikisha ujumbe kwa wanafunzi wa shule za msingi, Sekondari na vyuo vya kati ili wachukue tahadhari mapema na watu ambao wanaweza kuharibu ndoto zao.
Amesema sambamba na kampeni hiyo, pia wamefanikiwa kufanya jumla ya mikutano 113 ya uelimishaji kwa jamii na maeneo ya shule, na vikundi 27 vya ulinzi shirikishi ambayo vyenyewe vilipewa elimu ya ukamataji salama wa wahalifu kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu.
Pia, Jeshi hilo limewashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuendelea kudumisha aman na usalama, huku likitoa wito wasijihusishe na vikundi vibaya vyenye lengo la kuharibu amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwamba halitokuwa na muhali kwa yeyote atakaekwenda kinyume na sheria.
Uchaguzi huo wa serikali za mitaa utafanyika Novemba 27 mkwa huu, ambapo tayari zoezi la wananchi kujiandikisha kwenye daftari la makazi limeshakwisha tangu Oktoba 21.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464